Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amempa Waziri mpya wa TAMISEMI jukumu la kuhakikisha kuwa serikali yake chini ya Chama cha Mapinduzi CCM inanyakua ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika 2024 na ule uchaguzi mkuu utakaofanyika 2025.
Rais Samia ameeleza hayo leo Ikulu ndogo ya Visiwani Zanzibar wakati akiwaapisha vingozi wateule aliowateua Agosti 30,2023 ambapo pamoja na mambo mengine ameweka msisitizo wake kwa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa ambaye sasa amehamishiwa katika Wizara ya Tamisemi kuhakikisha anacheza karata zake vizuri ili ushindi urudi kwenye serikali yake.
Hii ni baada kuonyesha kufurahishwa na kazi alizozifanya Waziri Mchengerwa akiwa katika wizara zote alizowahi kuhudumia na kwamba amegeuka kuwa bingwa wa mageuzi.
Amesema amemhamishia katika Wizara hiyo ya TAMISEMI kwa kuwa mwaka kesho kutakuwa na kivumbi (Uchaguzi wa Serikali za Mitaa) ambacho anaamini ana kifua na atakimudu vizuri.
“Sasa nimempeleka (Mchengerwa) Tamisemi, mwakani kuna kivumbi na mimi nakujua najua unaweza, kivumbi kile kinafafanana na kifua chako najua unaweza kwa hiyo nimekupeleka Tamisemi ni kazi kazi ili mwakani tupite vizuri,” amesema Rais Samia.
Kabla ya Rais Samia kutoa kauli hiyo awali akizungumza katika hafla hiyo Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango amesema hatua ya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan Agosti 30, mwaka huu,ni safu ya kufunga magol
“Mheshimiwa Rais ameona ni vema apange safu ambayo inaweza kufunga magoli zaidi ili twende kuanzia mwaka kesho(2024) Uchaguzi katika Serikali za Mitaa na mwaka unaofuata (2025) Uchaguzi Mkuu twende tukafunge magoli ya uhakika sio ya kubabaisha”Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango
Pamoja na mambo mengine kwa upande wake Rais Samia amewaasa viongozi wote aliowateua kuwa kwa sasa Serikali pamoja na wananchi wote kwa ujumla wanachohitaji ni mabadiliko katika utendaji ili kuleta maendeleo.
“Makamu wa Rais amelisema vizuri sana ni kuhusu ‘Reform’ yaani mabadiliko, tunachotaka ni mabdiliko, tunayoahidi watu kila wakati, tunaahidi mambo mengi ili kuwaletea maendeleo, twendeni tukadilike,” amesema Rais Samia.
“Nitakapowachambua hapa nitawaambia mabingwa wa reforms, na pengine nimseme mmoja hapa, Mchengerwa kwa mfano nilipompeleka utumishi mwanzo namteua akaingia kwa kasi hadi kelele zikawa nyingi, nikasema labda Waziri wangu kazidi kapandisha mabega.
“Nikasema labda nimpeleke michezo, akaenda michezo kazi aliyofanya ninyi wenyewe mmeiona, kaacha kazi nzuri sana. Katoka michezo nimempeleka utalii… mipango aliyoiweka sekta ile, Angela (Kairuki), ukienda ukifuata yaliyowekwa utalii inakwenda kupanda juu.
Aidha amesema mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri aliyoyafanya hivi karibuni, si adhabu bali yanalenga kuimarisha maendeleo ya nchi.
“Lakini la pili mjue tu kwamba, mabadiliko haya ni adjustment. Maendeleo lazima yawe na bandika bandua, kaza nati fungua nati toa nati hii weka hapa. Ndiyo maana ya mabadiliko haya. Lakini tukikaa wenyewe nitawaeleza kwa undane. Nataka nisisitize kwamba, mabadiliko haya si adhabu, ni mabadiliko ya kawaida kuimarisha maeneo yetu,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amewataka viongozi kutii viapo vyao, pamoja na kujenga mahusiano mazuri na watendaji wengine katika wizara walizoteuliwa kufanyia kazi.
“Nataka nisisitize kwamba, mabadiliko haya si adhabu. Ni mabadiliko ya kawaida ya kuimarisha maeneo yetu. Ninachotarajia kwenu ni commitment kwenye kazi zenu. Ninyi ni watumishi wa umma sasa kuna mwingine akipata uteuzi sasa atanijua mimi nani? Kwa hiyo sisi ni watumishi wa watu na katika utumishi wa watu mahusiano ni jambo zuri sana,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema “Naombeni sana upole si ujinga hata kidogo, upole saa nyingine ndiyo maarifa. Unatulia, unafikiri jambo mara mbili tatu kabla hujatoa maamuzi. Kwa hiyo naomba mkatulie mtumikie watu.”