Rais Samia awaonya Wanaharakati, asema Tanzania haitasita kutumia nguvu kuhami raia wake

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaonya wanaharakati wote wanaojihusisha na shughuli za kuchochea vurugu nchini akisema kuwa wanachofanya ni ugaidi huku akienda mbali zaidi kwa kutafsiri neno Ugaidi.

Rais Samia amesema kundi hilo limekuwa likivaa sura za kizalendo lakini ndani yake wana maslahi binafsi ambapo wametumia fursa hiyo kutaka kubomoa nchi.

Ameyasema hayo leo wakati akishuhudia Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT- Wazalendo katika Viwanja vya Ikulu Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine Samia amewataka Watanzania kutoshawishika na kukubali kuibomoa nchi badala yake washikamane katika kuijenga

“Nawasihi Watanzania tushikamane kwa maendeleo ya taifa letu na sio kulifanya taifa kuwa duni kwa matakwa ya watu binafsi ambao maisha yao huko walipo na hata hapa nchini wanategemea malipo yatokanayo na kufaya vurugu au kuivuruga nchi yao kwa maslahi ya wengine” amesema Rais Samia.

 

Aidha amesisitiza kuwa Tanzania haitasita kutumia nguvu kama dola kuhami raia wake dhidi ya magaidi lakini si hivyo tu bali italinda heshima yake 

Vitendo vya Kigaidi havikubali sio kwa Tanzania bali ulimwengu mzima hivyo basi niwaonye wale wote wanaojishughulisha na vitendo hivyo kwamna taifa lolote dunaini hutumia nguvu ya dola kuhami raia wake na kulinda heshima yake nasi Tanzania kama taifa hatutasita kufanya hivyo” amesema Rais Samia.

Kauli ya Rais Samia imekuja siku mbili baada ya uwepo wa vuguvugu la maandamano ya Julai 7,2026 siku ya maadhimisho ya Sikukuu ya Saba Saba, maandamano ambayo chimbuko lake ni mitandaoni ingawa hayakufanyika.

Hivi karibuni nchini Tanzania  kumekuwa na maoni kinzani dhidi ya serikali kuhusu demokrasia, haki za binadamu na siasa kwa ujumla ambapo kundi la vijana la kizazi kipya maarufu Gen Z, limeonekana kuwa wakosoaji wakubwa wa Serikali wakiishinikiza kupata mabadiliko ya mifumo lakini na upatikanaji wa Katiba mpya.