Rais Samia awasili Ethiopia tayari kushiriki mkutano wa AU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole, Addis Ababa nchini Ethiopia leo  tarehe 14 Februari, 2025 kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa kawaida wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU). 

 

Ziara ya Rais Samia nchini Ethiopia imeanza leo ambapo anatarajia kuhitimisha Februari 16,2025.

 

Mkutano huo unatarajia kuchagua Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2025 atakayechukua nafasi ya Mwenyekiti wa sasa .

Aidha, Mkutano huo pia utachagua viongozi wapya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ikiwemo Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna sita.


Vilevile, Mkutano utajadili taarifa ya ushiriki wa Umoja wa Afrika kwenye mkutano wa nchi tajiri duniani (G20), utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na taarifa kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Mbali na masuala hayo, mkutano utajadili ajenda kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia iliyopendekezwa na  Tanzania.Kabla ya kushiriki Mkutano wa 38, Rais Samia atashiriki Mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika unaofanyika leo.