Rais Samia kununua magoli ya Simba na Yanga

Rais Samia Suluhu Hassan, ametangaza kununua kila goli litakalofungwa katika michezo ya kimataifa ya Simba na Yanga itakayochezwa mwishoni mwa wiki hii. 

Simba wanaoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, itashuka uwanjani Jumamosi ya tarehe 18 Februari, 2023 dhidi ya Raja Casablanca, wakati Yanga ambayo inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, itacheza na TP Mazembe ya DR Congo siku ya Jumapili zote katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Greyson Msigwa, amesema Rais Samia amefikia uamuzi huo ikiwa sehemu ya kuwapa hamasa timu hizo ili zifanye vizuri katika michuano hiyo ya kimataifa.

“Kila bao litakalofungwa kwenye michezo ya kimataifa itakayopigwa mwisho wa Juma hili, ambapo Simba na Yanga zitashuka dimbani, Rais wa Jahmhuri wa Muungano wa Tanzania atanunua kila bao kwa Shilingi Milioni 5, kama motisha,” amesema Msigwa.

Msigwa amesema Rais Samia anathamini mchango wa klabu hiyo kimataifa hivyo anaamini kuwa motisha hiyo itasaidia kuwasukuma wachezaji kufanya vizuri na kulitangaza taifa kwa ujumla.

Simba na Yanga ambazo zipo katika hatua ya makundi ya michuano hiyo zilipoteza michezo yao ya awali ambayo walicheza nje ya nchi.