Rais Samia kuunda tume mbili kuchunguza kinachoendelea Ngorongoro

Rais  Samia Suluhu Hassan amesema ataunda tume mbili kuchunguza kinachojiri eneo la Ngorongoro, kutokana na malalamiko ya wakazi wa eneo hilo yanayosababisha migogoro na vuta nikuvite baina ya Serikali na Wakazi.

Amesema tume moja itachunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro na nyingine itaangalia utekelezaji zoezi zima la uhamiaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Rais Samia ametoa kauli hiyo  jana katika Ikulu Ndogo ya Arusha wakati akizungumza na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimaasai (Malaigwanani) wanaoishi Ngorogoro lengo likiwa ni kuwasikiliza viongozi hao juu ya malalamiko hayo. 

Rais Samia aliwahakikishia serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya serikali na jamii hiyo.

Vilevile, alisisitiza ulazima wa wananchi kushirikishwa ipasavyo katika upangaji na utekelezaji miradi inayopita kwenye maeneo yao.

Rais Samia alisisitiza Tanzania ni nchi inayojivunia umoja wa kitaifa na yenye serikali inayowahudumia Watanzania wote. Hivyo, akaitaka Ofisi ya Rais – TAMISEMI kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwamo kukosekana baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la  Ngorongoro.

WANAHARAKATI WATOA NENO

Kauli ya Samia imepokewa tofauti kutoka kwa Wanaharakati wa Haki za Binadamu ambapo wametoa mashaka yao juu ya kauli hiyo wakisema kwamba si ya kushangiliwa kwa kuwa Tume nyingi zimeundwa lakini hazileti majibu kwa wananchi.

“Tunapongeza kwa hatua ya kukutana na watu wa Ngorongoro, imekuwa ni kilio cha muda mrefu, tumesisitiza akaonane na watu wake, huenda angekutana nao mapema zaidi yaliyotokea yasingetokea hivyo, ila tunashukuru angalau amekutana nao,” alisema Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (THRDC), Dk. Anna Henga, alisema kuunda tume si kitu cha kushangiliwa sana, bali ni matokeo ya tume kuwa wazi na kufanyiwa kazi. Alitahadharisha kuwa tume nyingi zinaundwa na zinatoa mapendekezo, lakini hayafanyiwi kazi.

“Sifurahii sana tume ikiundwa, ninaona ni kunyamazishwa, huwa sioni matokeo ya tume hizi. Ngorongoro kuna changamoto kubwa, kama kweli watafanya kazi watakuja na mapendekezo yanayotekelezeka kabisa,” alisema.