Rais Samia shtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa Madai ya Uhalifu Dhidi ya Ubinadamu

Tanzania inakabiliwa na kile kinachoelezwa kama janga kubwa la kibinadamu, kufuatia madai ya uhalifu wa kimfumo na wa kiwango kikubwa dhidi ya ubinadamu unaodaiwa kufanywa na vyombo vya usalama vya serikali. 

Waathiriwa wakiwemo waandamanaji, wanaharakati, waandishi wa habari na jamii za kiasili kama Wamaasai, wanadaiwa kukumbwa na mauaji ya kikatili,, utekaji wa lazima, na mateso.

Kwa mujibu wa ombi lililowasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), vyombo vya usalama vya Tanzania “vimeua maelfu ya raia, kuwateka kwa lazima mamia ya watu, kutesa maelfu katika vituo vya polisi, kufanya ukatili wa kingono dhidi ya mahabusu, kuwahamisha kwa nguvu makumi ya maelfu ya Wamaasai, na kutumia mbinu za ukandamizaji wa kidijitali zinazowaathiri mamilioni.” Mashambulio haya yanadaiwa kuwa ya maeneo mengi takriban mikoa tisa na, yakiendelea kwa miaka tangu 2016.

Mwasilishaji wa ombi hilo, wakili Juan Carlos Gutierrez, anayewakilisha waathiriwa, anadai kwamba Rais Samia Suluhu Hassan, kama Amiri Jeshi Mkuu, anabeba jukumu la mwisho kwa madai hayo, akisema aliidhinisha moja kwa moja matumizi ya nguvu dhidi ya raia.

Gutierrez anaeleza kuwa uhusiano na utaratibu wa mashambulio unaonekana kupitia mipango ya pamoja, mifumo inayojirudia ya ukatili, pamoja na matumizi ya sheria na mifumo ya kisheria kuhalalisha uhalifu nchini. Anasema uhalifu uliotajwa katika ombi hilo unaangukia chini ya Kifungu cha 7 cha Mkataba wa Roma, ikiwemo mauaji, maangamizi, utekaji wa lazima, mateso, ubakaji, na mateso ya kimfumo dhidi ya makundi maalumu.

ICC ina mamlaka ya kushughulikia suala hilo kwa kuwa Tanzania ni Mwanachama wa Mkataba wa Roma, na kwa kuwa uhalifu ulidaiwa kufanyika ndani ya ardhi ya Tanzania. Ombi hilo linaiomba ICC kuanzisha uchunguzi wa awali na kuomba idhini ya kufungua uchunguzi wa kina.

Katika waraka wake wa kurasa 85 aliomwasilisha kwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa ICC, Karim Khan, Gutierrez ameambatisha video na picha ambazo anasema zinathibitisha madai ya mauaji ya wingi wakati na baada ya uchaguzi wenye utata uliofanyika tarehe 29 Novemba 2025.

Gutierrez pia ametaja orodha ya zaidi ya watu 200 wanaodaiwa kupotezwa nchini Tanzania chini ya utawala wa Suluhu.

Alisema:

“Athari zinakwenda zaidi ya waathiriwa wa moja kwa moja:

Uharibifu wa Upinzani: Kuondolewa kwa kimfumo uwezo wa vyama vya upinzani kufanya kazi; kufungwa kwa viongozi; kuuawa kwa waandamanaji.

Kutishwa kwa Asasi za Kiraia: Watetezi wa haki za binadamu, waandishi na wanaharakati kukabiliwa na tishio la kudumu la kutekwa, kuteswa au kuuawa; kuzimwa kwa ushiriki wa kiraia.

 Uhamishaji wa lazima wa Wamaasai 80,000–150,000 unafanana na usafishaji wa kikabila; uharibifu wa utamaduni na maisha ya jamii za kiasili.

Msongo wa Vizazi: Watoto waliotazama ukatili au kupoteza wazazi watabeba maumivu ya muda mrefu; jamii zilizoathiriwa na operesheni za Kibiti zimeharibiwa kabisa.

Kuvurugika kwa Utawala wa Sheria: Kuporomoka kwa uhuru wa mahakama na uwajibikaji, na kuacha utamaduni wa kutoadhibiwa.

Hali hiyo nchini Tanzania imezua wasiwasi wa kimataifa, huku Umoja wa Mataifa, Amnesty International na Human Rights Watch wakilaani kile kinachoelezwa kama ukatili unaoendelea. 

Ombi hilo linaeleza kuwa “wakati wa kuchukua hatua ni sasa,” likiongeza kuwa waathiriwa nchini Tanzania “wamesubiri haki kwa muda mrefu. Kila siku ya kuchelewa ni siku nyingine ya ukosefu wa uwajibikaji, siku nyingine ya kuendelea kwa uhalifu, siku nyingine ya ushahidi kuharibiwa na siku nyingine ya mashahidi kutishwa.”

Madai hayo yanajumuisha ukatili wa baada ya uchaguzi, ukiwemo madai ya mauaji ya wengi, utekaji wa lazima na mateso. Kuzimwa kwa mtandao katika kipindi hicho kunadaiwa kuwezesha uhalifu huo, huku matumizi mabaya ya Sheria ya Makosa ya Mtandao yakitoa msingi wa ukandamizaji wa kidijitali.

Ombi hilo linasisitiza umuhimu wa kuchukua hatua haraka, kwa maelezo kuwa ushahidi unaendelea kupotea, mashahidi wanatishwa, na waathiriwa wanaendelea kupata madhila. Gutierrez anataka ICC ichukue hatua za haraka ili kuhakikisha uwajibikaji na kuleta tumaini kwa waathiriwa wa madhila hayo