Rais Samia:Sekta binafsi ifanye biashara serikali itabaki kama msimamizi

Rais  wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameweka wazi kuwa sera ya utawala wake ni kuiacha sekta binafsi kufanya biashara na Serikali kubakia kama msimamizi. 

Rais Samia ameyasema hayo leo  wakati akizungumza katika kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Oman lililofanyika Ikulu ya Oman.

Mkuu huyo wa nchi yupo ziarani nchini Oman kwa mwaliko wa Mfalme, Haitham Bin Tariq kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili zenye historia ya muda mrefu.

Amesema Tanzania imejidhatiti kuwa na uchumi unaoendeshwa na sekta binafsi na Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara “kwa kushirikiana na sekta binafsi tunakwenda kuunda sera ya ushindani wa sekta binafsi,”

“Tangu nimeingia madarakani sera yangu imekuwa ni acha Serikali iwe msimamizi na sekta binafsi ifanye biashara, namaanisha kwamba hakuna tena biashara Serikalini, sekta binafsi itafanya biashara na Serikali sisi tunatengeneza mazingira rafiki kwa uwekezaji wa ndani au nje, hiyo ndiyo sera yangu,” amesema Rais Samia.

Amesema Tanzania “inatambua kazi kubwa” inayofanywa na wawekezaji katika kukuza uchumi na kutoa ajira “na ili kuchagiza uwekezaji wa ndani na wa nje tumejitahidi kuwa na sera Rafiki kwa uwekezaji na ufanyaji biashara.”

“Natambua kumekuwa na changamoto lakini nipo hapa na nawahakikishia nitakwenda kurekebisha chochote kilichowahi kutokea huko nyuma na tutakwenda kufanya kazi pamoja na kufanya uwekezaji kwa pande zote za nchi zetu,” amesema Rais Samia.

Amesema wamekuwa na mkakati wa kubadilisha kanuni za ufanyaji biashara na kwa kushirikiana na Mamlaka za za kodi wameondoa kodi nyingi zisizo na tija.