Rais wa Cameroon, Paul Biya, ametangaza Jumapili kwamba atagombea tena urais kwa muhula wa nane katika uchaguzi wa Oktoba, hatua itakayoongeza utawala wake ambao umedumu kwa takriban miaka 43.
Biya, mwenye umri wa miaka 92, alitoa tangazo hilo kupitia mtandao wa X kwa lugha ya Kifaransa na Kiingereza.
“Ninagombea katika uchaguzi wa urais wa tarehe 12 Oktoba 2025. Hakikisheni kuwa nia yangu ya kuwatumikia inalingana na changamoto kubwa zinazotukabili,” aliandika.
“Pamoja, hakuna changamoto tusiyoweza kukabiliana nayo. Mema bado yanakuja.”
Biya tayari alikuwa anachukuliwa kama mgombea rasmi wa Chama cha Cameroon People’s Democratic Movement (CPDM), ambacho yeye ndiye kiongozi wake.
Hata hivyo, kutokana na umri wake mkubwa, afya yake na uwezo wa kuendelea kuongoza vimezua mijadala mikali.
Baadhi ya wafuasi wake wa muda mrefu wameanza kujitenga naye katika miezi ya hivi karibuni, huku kukiwa na wanachama wawili waandamizi waliotangaza kuondoka kwenye kambi ya Biya.
Waziri wa Ajira, Issa Tchiroma Bakary, alijiuzulu mwezi Juni ili kugombea urais kupitia chama chake cha Front for the National Salvation of Cameroon (FSNC).
Kadhalika, Waziri Mkuu wa zamani, Bello Bouba Maigari, ambaye amekuwa mshirika wa Biya kwa karibu miaka 30, ametangaza kugombea urais kupitia chama cha National Union for Democracy and Progress (NUDP).
Vyama vya Tchiroma na Maigari vimekuwa washirika wa muda mrefu wa chama tawala cha CPDM, ambacho kimeshikilia madaraka tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1960.
Wagombea wengine waliotangaza nia ya kugombea ni pamoja na Maurice Kamto, aliyeshika nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2018 na ambaye ni mpinzani mkubwa wa Biya, pamoja na Cabral Libii kutoka chama cha Cameroonian Party for National Reconciliation (CPNR).
Wagombea wote wana hadi tarehe 21 Julai kutangaza rasmi nia ya kugombea urais.
Hata hivyo, upinzani umegawanyika vibaya na umeshindwa kuungana nyuma ya mgombea mmoja licha ya kuwepo kwa malalamiko makubwa ya wananchi dhidi ya serikali.
Raia wa Cameroon hulalamikia kwa kiasi kikubwa ukosefu wa ajira kwa vijana, kupanda kwa gharama za maisha na huduma duni za umma.
Aidha, ghasia za mara kwa mara kutoka kwa wanaharakati wa kujitenga hujitokeza hasa katika maeneo yanayozungumza Kiingereza kwenye nchi hiyo inayotawaliwa kwa kiasi kikubwa na wanaozungumza Kifaransa.