Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi amemteua kiongozi wa zamani wa wanamgambo Jean-Pierre Bemba kuwa waziri wa ulinzi katika mabadiliko ya baraza la mawaziri siku ya Ijumaa, wakati nchi hiyo ikikabiliana na mzozo wa kivita mashariki mwake.
Bemba, ambaye aliwahi kuwa makamu wa rais kutoka 2003 hadi 2006, alikuwa amefungwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa uhalifu uliofanywa na waasi chini ya amri yake, lakini mahakama hiyo ilibatilisha hukumu yake mwaka 2018.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inajitahidi kuzima uasi wenye silaha unaofanywa na waasi wa M23, ambao Kinshasa na serikali kadhaa za Magharibi zinasema kuwa inaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda.
Mkuu wa zamani wa Tshisekedi, Vital Kamerhe, aliteuliwa kuwa waziri wa uchumi, baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa utakatishaji fedha kabla ya kuachiliwa huru mwaka jana.
Msemaji wa Tshisekedi alionekana kwenye televisheni ya taifa mapema Ijumaa kusoma muundo wa serikali mpya.
Nchi inatazamiwa kupiga kura mnamo Desemba.
Tshisekedi, ambaye amekuwa madarakani tangu Januari 2019, amesema atawania tena uchaguzi huo.