Rais wa zamani wa Algeria Abdelaziz Bouteflika, aliyepigania uhuru wa taifa lake kutoka kwa ukoloni wa Ufaransa ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 84.
Abdelaziz Bouteflika,alikuwa rais wa Algeria kwa miaka 20 kutoka mwaka 1999 hadi 2019 alipojiuzulu.
Bouteflika alihudumu katika jeshi la Ukombozi wa Algeria (NLFA) katika vita vya kumuondoa mkoloni. Baada ya Algeria kupata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa, alihudumu kama Waziri wa Mambo ya nje kati ya 1963 hadi 1979.
Mwaka wa 1999 alichaguliwa kuwa Rais wa Algeria, na akashinda uchaguzi wa 2004, 2009 na 2014. Bouteflika alijiuzulu tarehe 2 Aprili 2019 baada ya miezi mingi ya maandamano.
Bouteflika aliiongoza Algeria kwa miaka 20, ndiye kiongozi ambaye amehudumu kwa muda mrefu kama rais nchini humo.
Bouteflika alikuwa amepata kiharusi mnamo 2013 ugonjwa ambao ulimdhoofisha sana, wasiwasi juu ya hali yake ya afya, ulifichwa kutoka kwa wananchi. Maandamano yaliyoongozwa na kundi la Hirak yalimfanya akajiuzulu na kumaliza uongozi wake
wa miaka 20.
Taarifa kutoka kwa ofisi ya Rais wa sasa Abdelmadjid Tebboune, haikutoa sababu ya kifo chake au habari zozote kuhusu mipango ya mazishi yake.