Ripoti ya ajali ya ndege iliyokanwa na Serikali ya Tanzania yafanania na ripoti rasmi iliyotolewa.

Wakati joto likiendelea kuongezeka juu ya ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, ambayo Serikali ya Tanzania iliikana ripoti hiyo, hapo jana Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi nchini humo, Profesa Makame Mbarawa ametoa taarifa rasmi ya ripoti ya uchunguzi huo wa awali ambayo kwa namna moja ama nyingine haina tofauti sana na ripoti iliyokataliwa na Serikali.

Jana  Alhamsi Novemba 24, 2020 akisoma taarifa rasmi ya ripoti ya uchunguzi huo wa awali, Profesa Mbarawa amesema hali ya hewa ya Bukoba ilikuwa nzuri hadi Saa 2 na dakika 20 asubuhi, taarifa ambayo hivyohivyo imeonyesha katika ripoti iliyokanwa na Serikali 

“Lakini ilibadilika ghafla kwa mvua kuanza kunyesha ikiambatana na ngurumo za radi, upepo mkali na mawingu na ndege hiyo iliingia katika anga la Bukoba saa 2 na dakika 25 asubuhi na kukutana hali ya hewa hiyo. Ndege ilizunguka kwa dakika 20 ikitarajia hali ya hewa kubadilika na kuwa nzuri, baadaye rubani alianza maandalizi ya kutua kutokea upande wa ziwa.

“Kutokana na maelezo ya abiria walionusurika na ajali, walisema njia ya kutua na kuruka ndege ilikuwa inaonekana. Haya ni maelezo ya watu waliokuwa ndani ya ndege na mashuhuda wengine,” amesema Profesa Mbarawa.

Akiendelea kuisoma ripoti rasmi ya Serikali, Profesa Mbarawa naye alisema “ripoti inaeleza kuwa  mlango wa ndege ulifunguliwa na muhudumu wa ndege kwa msaada wa abiria.”

Hii haiko tofauti sana na kile kilichoandikwa kwenye ripoti iliyokataliwa na Serikali ambayo inatajwa kuwa sio ripoti rasmi.

Katika ripoti iliyosambaa mitandaoni ambayo Serikali imeikana, imeeleza kuwa muhudumu mmoja ndiye aliyefungua mlango wa kushoto wa abiria, akisaidiwa na abiria mmoja kuusukuma. Baadhi ya manusura, akiwemo mtoto mwenye miezi 18 na mama yake waliokolewa kwa njia hiyo.

Hata hivyo, waziri huyo amesema wananchi waliokuwa wakifanya shughuli za uokozi walifika eneo la tukio baada ya dakika tano ndege hiyo kuanguka, kauli ambayo imo kwenye ripoti iliyokanwa na Msemaji mkuu wa Serikali kuwa si rasmi na ipuuzwe.

Jana  Waziri Mbarawa alisema; “Wananchi hawa waliendelea na jitihada za kufungua mlango kwa nje, hali iliyompa ujasiri muhudumu wa ndege na abiria kuufungua mlango baada ya kuona nje ya ndege kuna msaada,” amesema Profesa Mbarawa.

Akizungumzia kuchelewa kwa vyombo vya uokozi, Profesa Mbarawa amesema katika ajali zinazotokea majini ipo miongozo na taratibu za kimataifa kuhusu uendeshaji wa mchakato huo na inayongozwa na mkataba wa kimataifa wa namna ya utafutaji na uokoaji majini wa mwaka 1974 ambao Tanzania imeridhia.

“Mkataba huu umetoa mwongozo kwamba, pale inapotokea ajali katika maji ya ziwa au bahari, inamtaka mtu au kikundi cha watu waliopo karibu na eneo la ajali kuwajibika na uokozi na kutoa taarifa kwa vyombo husika.

“Watu hawa wanawajibika kuendelea na uokozi hata pale inapotokea vyombo vya uokoaji vinavyofika katika eneo la ajali, huu ndio mwongozo sahihi unaotolewa na unaendana na utamaduni wetu kwamba, inapotokea ajali watu walio karibu husaidia kuwakoa manusura,” amesema.

Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, wavuvi walioshiriki katika mchakato wa uokozi kwenye ajali hiyo ya ndege, walitimiza wajibu wa kizalendo na suala hilo linakubalika kimataifa.

Kuhusu Majaliwa (Jackson) kuwa shujaa, Profesa Mbarawa amesema “katika ripoti haikutaja mtu jina, bali imewatambua wavuvi hata mhuhudumu imesema muhudumu wa ndege haikutaja jina. Nimekuja hapa kuripoti kile kilichosemwa na kwenye ripoti.”

Itakumbukwa kuwa Majaliwa ni miongoni mwa vijana waliowaokoa abiria wa ajali ya ndege hiyo.

https://mwanzotv.com/2022/11/24/tanzania-yaikana-ripoti-ya-awali-ya-ajali-ya-ndege-bukoba/