Rostam Aziz mmiliki mpya wa kampuni ya habari ya Nation Media Group

Mfanyabiashara mashuhuri wa Afrika Mashariki, Rostam Aziz, sasa amekuwa miongoni mwa wawekezaji wakubwa katika sekta ya habari baada ya kuwa mbia mkuu wa kampuni ya habari ya Nation Media Group (NMG).

Hatua hiyo imekuja kufuatia uamuzi wa Aga Khan Fund for Economic Development (AKFED) kuuza hisa zake zote zilizokuwa zikimilikiwa katika kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Jumanne, Machi 10, 2026, AKFED imefikia makubaliano ya kuuza umiliki wake wa asilimia 100 katika kampuni ya NPRT Holdings Africa Limited kwa kampuni ya Taarifa Ltd, inayomilikiwa na Rostam Azizi.

Mabadiliko hayo yanaashiria hatua mpya katika umiliki wa moja ya makampuni makubwa zaidi ya habari katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Nation Media Group (NMG) ni mojawapo ya makampuni makubwa ya vyombo vya habari katika eneo hilo, ikiwa inafanya kazi katika nchi za Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda.

Kampuni hiyo inachapisha magazeti kadhaa maarufu ikiwemo Daily Nation, Sunday Nation,The EastAfrican, Daily Monitor ya Uganda, pamoja na Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti nchini Tanzania.

Mbali na magazeti, NMG pia inamiliki NTV Kenya na NTV Uganda, pamoja na mtandao wa vituo vya redio vinavyofanya kazi katika nchi za Kenya, Uganda na Rwanda.