Search
Close this search box.
Africa
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Wankyo Nyigesa.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania , IGP Simon Sirro amemrejesha Makao Makuu ya Polisi, Dodoma Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Wankyo Nyigesa.

Mabadiliko hayo yamefanyika leo, ambapo nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), William Mwampagale

Uhamisho huo umefanyika ili kupisha uchunguzi wa tukio lililotokea Machi 26, 2022 katika sherehe ya kumuaga Nyigesa ambaye alihamishwa kutoka Pwani kwenda Kagera, na nafasi yake kuchukuliwa na Pius Tuli.

Kwa mujibu wa Polisi nchini Tanzania, maneno aliyoyatoa yameonesha ukiukwaji wa nidhamu kulingana na miongozo ya Jeshi la Polisi humo, na kwamba suala hilo limeanza kufanyiwa kazi na hatua zaidi zitachukuliwa.

Hata hivyo katika taarifa hiyo iliyotolewa leo na Jeshi la Polisi haijaeleza maneno yaliyotolewa, lakini hivi karibuni kamanda huyo alisikia akisema kwamba sasa anajiandaa kuwa IGP.

“Mimi huwa ninajiandaa kuwa DCI Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai lakini nafasi ya DCI ikachukuliwa, nikajiandaa kuwa Kamishna wa Zanzibar, Kamishna wa Zanzibar wakachukua, sasa hivi najiandaa kuwa IGP,” alisema Wankyo.

Kufuatia mabadiliko hayo, aliyekuwa Afisa Mnadhimu Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Theopista Mally anakuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo.

Comments are closed