,

Ruto Awakaba Koo Wapinzani: “Kenya inahitaji Kiongozi Mwenye Akili”

Victor Wanaswa Avatar

Rais William Ruto amewashambulia viongozi wa upinzani watakaokabiliana naye katika kinyang’anyiro cha kuelekea Ikulu mwakani, akisema Kenya ni nchi ya kisasa na yenye masuala na changamoto nyingi hivyo inahitaki kiongozi mwenye akili na uelewa wa kina ili kuiendesha.

Akizungumza wakati wa hafla ya Mahafali ya Mamlaka ya Kitaifa ya Mafunzo ya Viwanda (NITA) katika Ikulu ya Nairobi, Ruto alisema baadhi ya wanaowania urais wanatafuta nafasi hiyo bila kuelewa kikamilifu majukumu na changamoto zinazohusika katika kuiongoza taifa.

“Ninawaona wengi wakikimbia huku na huko. Kenya ni nchi ya kisasa, yenye masuala mengi na changamoto nyingi. Hakuna mjinga anayeweza kuiongoza nchi hii,” alisema Ruto.

Rais aliyekuwa akitetea kushiriki kwake katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA), amesema hadhi na heshima ya Kenya katika jukwaa la kimataifa ni ya kupigiwa mfano. Aliongeza kuwa nchi inahitaji kiongozi mwenye akili ili kuisukuma mbele.

Ruto amekuwa akitumia lugha ya matusi dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa, akiwashutumu kwa kukosa akili, mipango, mwelekeo na suluhisho mbadala kwa changamoto zinazoikabili Kenya.

Rais amekuwa akielezea kuwa serikali yake ina mkakati inayolenga kutekeleza miradi na ahadi zake kwa wakenya, huku akiitaja upinzani kama upande ulioshindwa kuwaeleza wakenya sera mbadala za kuendeleza taifa.

Katika mkutano wa hadhara kaunti ya Kajiado Septemba 3, Ruto aliwataka viongozi wa upinzani kuwasilisha ajenda, sera, mipango na maono yao badala ya kujikita katika mashambulizi ya kisiasa.

“Mimi nawaambia wale viongozi wengine, kila mtu wacha kuja kutupea ufala. Usituletee kelele, sisi ni watu tuko na akili,” alisema Ruto.

Katika hotuba yake kwa wahitimu, Rais aliwataka pia kuthamini ujuzi waliopokea na kutokubali kulipwa mishahara duni kwa kazi wanazofanya.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Our Correspondent Avatar