Manusura wa mauaji ya halaiki ya Rwanda Jumanne walipongeza uamuzi wa mahakama ya Umoja wa Mataifa kumpeleka Felicien Kabuga mahakamani, baada ya mawakili wake kushindwa kusitisha kesi dhidi yake kwa misingi ya afya.
Kabuga mwenye umri wa maika 87, anayedaiwa kuwa mfadhili wa mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 ambayo yalisababisha vifo vya watu 800,000 hasa Watutsi, anatuhumiwa kusaidia kuunda kundi la wanamgambo wa Kihutu wa Interahamwe, kundi kuu lenye silaha lililohusika katika mauaji hayo, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Alikamatwa Mei 2020 katika kitongoji cha Paris baada ya kutoroka kwa miaka 25 na kwa sasa yuko kizuizini huko The Hague akingojea kesi yake mbele ya Mechanism for International Criminal Tribunals (MICT).
“Walionusurika katika mauaji ya halaiki wamefurahishwa na uamuzi kwamba Felicien Kabuga anafaa kushtakiwa. Umri na udhaifu haviondoi hitaji la uwajibikaji,” Freddy Mutanguha, makamu wa rais wa Ibuka, kikundi kikuu cha msaada kwa manusura wa mauaji hayo.
“Pamoja na manusura wa mauaji ya halaiki dhidi ya Watutsi kila mahali, tunatarajia haki kutendeka,” Mutanguha aliambia AFP.
Wataalamu mbalimbali walihusika katika kuandaa kesi hiyo, ambayo, “inadhihirisha bila shaka kwamba Kabuga yuko katika mazingira magumu na tete na anahitaji huduma za matibabu na ufuatiliaji,” MICT ilisema Jumatatu.
MICT ilisema ni kwa manufaa ya haki kwa kesi hiyo kuanza haraka iwezekanavyo huko The Hague.
Maoni ya wataalam huru wa uchunguzi yalitofautiana kuhusu iwapo Kabuga anaweza kujibu mashtaka, lakini walikubaliana kuwa hali yake inaweza kumfanya asiwe sawa katika siku zijazo, mahakama hiyo ilisema.
Anahitaji “huduma ya uuguzi ya saa 24” na kwa sasa anaishi katika hospitali ya magereza, iliongeza.
Kabuga, rais wa zamani wa Radio Television Libre des Mille Collines (RTLM), ambayo inatangaza wito wa kuuawa kwa Watutsi, anatuhumiwa na MICT kwa mauaji ya kimbari, uchochezi wa mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
MICT inakamilisha kazi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya Rwanda.