Aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya amefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza akiwa pekee yake, baada ya washtakiwa wenzake wanne kuachiwa huru wiki iliyopita.
Sabaya amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, mbele ya Hakimu Salome Mshasha akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba mbili ya mwaka 2022.
Washtakiwa wengine wanne waliokuwa na Sabaya katika kesi hiyo, waliachiwa huru baada ya kukiri makosa yao na kutiwa hatiani.
Washtakiwa hao ni Silvester Nyegu ambaye alikuwa msaidizi wa Sabaya, John Odemba, Nathan Msuya na Assey ambao ni wafanyabiashara.
Pia walitakiwa kulipa faini ya shilingi elfu 50,000 kila mmoja kwa makosa mawili pamoja na fidia ya shilingi milioni moja kila mmoja kwa muathirika wa tukio hilo.