Search
Close this search box.
Africa

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (35) na wenzake sita wameachiwa huru.

Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda, leo Ijumaa Juni 10, 2022 amewaachia huru washitakiwa hao baada ya kubaini kuwa ushahidi wa mashahidi 13 upande Jamhuri ulikuwa ukikinzana na pia hati ya mashitaka iliyosomwa mahakamani ilikuwa na kasoro nyingi.

Kisinda alianza kusoma hukumu hiyo saa 4: 36 asubuhi  na kumaliza saa 7:45 mchana, alisema ushahidi wa mashahidi 13 wa upande wa Jamhuri ulikuwa ukikinzana dhidi ya watuhumiwa waliofunguliwa kesi ya uhujumu uchumi .

Kutokana na hali hiyo amesema, Mahakama imeamua kuwaachia huru watuhumiwa wote kwa kuwa hakuna ushahidi uliothibitisha pasipo shaka kuwa watuhumiwa hao wametenda makosa hayo.

Hakimu Kisinda alisema mbali ya kujikanganya kwa mashahidi hao, pia hati ya mashitaka ilikuwa na kasoro nyingi zilizotoa mwanya kwa watuhumiwa kuachiwa na mahakama.

‘’Ninawaachia huru watuhumiwa wote katika kesi hii ya uhujumu uchumi na kama upande wowote haujaridhika kuna nafasi ya kukata rufaa,’’alisema Hakimu Kisinda. 

Hii ni kesi ya pili Sabaya kushinda ambapo Mei 6, 2022 na wenzake wawili Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, walishinda rufaa iliyokuwa ikisikilizwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, waliyokata kupinga hukumu ya miaka 30 iliyokuwa imetolewa na na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Mbali ya Sabaya Watuhumiwa wengine walioachiwa huru katika kesi hiyo ni Enock Mnkeni (41) ,Watson Mwahomange (27), John Aweyo (45), Sylivester Nyegu (26), Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31). 

Hata hivyo Sabaya, Aweyo, Nyengu na Msuya bado wanakabiliwa na kesi nyingine Mjini Moshi, hivyo wameondoka chini ya ulinzi wa askari Magereza na kusafirishwa kwenda Gereza Kuu la Karanga lililopo katika Mji wa Moshi.

https://mwanzotv.com/2022/06/10/hukumu-katika-kesi-ya-uhujumu-uchumi-inayomkabili-sabaya-na-wenzake-kutolewa-leo/

Comments are closed