Wiki hii ilikuwa ni wiki ya hekaheka za vikao vya kamati kuu vya chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, ambayo imeishia katika mkutano mkuu wa chama hicho ambao ulitambulisha safu ya viongozi wapya ikiwa ni sehehmu ya kupokezana kijiti kama ambavyo Katiba yao inawataka kufanya hivyo kila inapofika miaka mitano.
Wajumbe takribani 586 walikutana katika ukumbi maarufu wa mikutano wa Mlimani City, na kushiriki uchaguzi wa ndani ya chama ili kupata safu ya viongozi ambao watakipeleka chama kwenye maono wanayoyataka.
Katika uchaguzi huo wajumbe walimuidhinisha na kumpa kibali cha kuongoza chama hicho kama Kiongozi wa chama bi Dorothy Semu ambaye alipata kura 354 sawa na asilimia 65.7 ya kura zote zilizopigwa, dhidi ya mpinzani wake Mbarala Maharagande aliyepata kura 184 au 34.3 .
Itakumbukwa kuwa nafasi ya Kiongozi wa chama ama kama wenyewe wanavyopenda kuita KC, ni nafasi ya juu kabisa ndani ya chama cha ACT Wazalendo ambayo ndiyo inabeba jukumu kubwa la kupambania chama na kukifikisha mahali wanachama wanahitaji.
Dorothy anashika wadhifa huo akipokea kijiti kutoka kwa aliyekuwa Kiongozi wa ACT Wazalendo ndugu Zitto Kabwe aliyehudumu katika nafasi hiyo kwa takribani miaka 9, ambaye sasa anabaki kama mshauri wa chama kwa mujibu wa Katiba ya ACT Wazalendo.
Wajumbe pia walimchagua Othman Masoud Othman, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho kitaifa, akimrithi mwanasiasa mkongwe Juma Duni Haji ambaye alijiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho mwishoni mwa kipindi cha kampeni, akisema anataka kudumisha “umoja wa chama” wakati wa mchakato huo.
Othman, aliyepata kura 96.6 za NDIYO kati ya kura zote 536 zilizopigwa, atasaidiwa na Ismail Jussa, ambaye anakuwa Makamu Mwenyekiti mpya wa chama kwa upande wa Zanzibar na Isihaka Mchinjita, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Tanzania Bara.
Hii leo halmashauri kuu ya chama hicho inaendelea na vikao vyake ambapo pamoja na mambo mengine itakuwa na kazi ya kuwathibitisha viongozi wapya waliochaguliwa huku ikitarajiwa kumchagua Katibu Mkuu wa chama pamoja na viongozi wengine wa kanda waliochaguliwa wakati wa mkutano huo.
Katika hotuba zao kwa wanachama viongozi hao wamekuwa wakisisitizia suala la uchaguzi kwa kile walichokieleza ni kutaka kuhakikisha chama kinashika dola katika uchaguzi mkuu wa mwakani lakini pia kushika nafasi nyingi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu.
Watanzania watapiga kura mwishoni mwa mwaka huu kuchagua wenyeviti wao wa mitaa au vijiji. Mwaka 2025, watawapigia kura marais wa Tanzania na Zanzibar, wabunge wa Bunge na Baraza la Wawakilishi na madiwani Zanzibar. ACT-Wazalendo inataka kufanya vyema katika uchaguzi huo, na viongozi wapya waliochaguliwa wanatarajiwa kuhakikisha hilo linafanyika.
Chama cha ACT Wazalendo kilianzishwa mnamo mwaka 2014 na ni chama kinachoendelea kukua kwa kasi nchini Tanzania. Kimejinasibu kama vuguvugu lenye lengo la kutengeneza Tanzania huru, yenye maendeleo na mafanikio ambayo misingi yake itakuwa ni uhuru, uwajibikaji, na uwazi.