Samia akiri ghasia za uchaguzi zimeiathiri Tanzania Kimataifa, ahofia kutopata mikopo

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekiri hadharani kwamba ghasia za maandamano zilizotokea siku ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, na siku zilizofuata, zimetia doa taswira ya taifa na huenda zikapunguza sifa ya nchi kupata mikopo kutoka taasisi za Kimataifa.

Ametoa kauli hiyo Novemba 17, 2025, akiwa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, muda mfupi baada ya kuapisha baraza jipya la mawaziri alilolitangaza siku iliyotangulia.

Rais Samia amesema Tanzania kwa kiasi kikubwa bado inategemea mikopo kutoka taasisi za Kimataifa ili kuendeleza miradi yake ya maendeleo. Hata hivyo, kutokana na matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi, huenda taasisi hizo zikapungukiwa na imani ya kuifadhili Tanzania. Ameeleza kuwa sasa ni muhimu kutafuta mbinu mbadala za kupata fedha, ikiwemo kutumia rasilimali za taifa zilizo ndani ya nchi.

“Changamoto nyingine inayotukabili ni rasilimali. Rasilimali zetu ni chache kama mnavyojua, na mara nyingi tunategemea kupata kutoka nje kupitia mikopo ya taasisi mbalimbali za Kimataifa na mabenki ya Kimataifa. Lakini yaliyotokea nchini kwetu yametutia doa, hivyo huenda yakatupunguzia sifa ya kupata mikopo kwa urahisi kama ilivyokuwa katika muhula wa kwanza wa awamu hii. Tulipata sana kwa sababu ya sifa zetu, msimamo wetu na kazi tulizokuwa tukifanya, lakini doa tulilojitia huenda likaturudisha nyuma,” amesema Rais Samia.

Amesisitiza kuwa miradi ya maendeleo haiwezi kusubiri wadau wa nje, hivyo ni lazima kuitekeleza kwa wakati kupitia juhudi za ndani. Amewataka mawaziri aliowateua kupambana kikamilifu kutafuta njia za kupata fedha za kutekeleza miradi waliyoiahidi kwa wananchi.

“Kwa hiyo tunayo kazi ya kutafuta fedha humu ndani, kutumia rasilimali alizotupa Mungu. Tutaangalia ni njia gani tutumie ili kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi yetu,” amesisitiza.

Tanzania ilikumbwa na ghasia za maandamano kwa takribani siku tatu mfululizo kuanzia Oktoba 29, 2025, katika maeneo mbalimbali, hasa katika majiji makubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mwanza.

Inakadiriwa kuwa mamia ya vijana walioshiriki maandamano hayo waliuawa kwa kupigwa risasi na vyombo vya dola, huku zaidi ya watu 500 wakifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya Uhaini, ambayo adhabu yake kisheria ni kifo.

Hata hivyo, Novemba 14, 2025, wakati akilihutubia Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia alitangaza msamaha kwa baadhi ya vijana hao na kuziagiza mamlaka za ulinzi kutafuta namna ya kuwaachia, akibainisha kuwa wengine walijikuta wakifuata mkumbo.

Matukio haya yameitikisa Tanzania kisiasa na kuathiri kwa kiasi kikubwa taswira ya taifa kimataifa, huku kukiwa na ukosoaji mkubwa dhidi ya utawala wa Rais Samia, ambao unashutumiwa kwa kukandamiza demokrasia na haki za binadamu.