Samia amtaka Waziri kumpatia ripoti ya Kariakoo kila baada ya miezi mitatu

Rais  Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo kwenda ‘kushinda’ Kariakoo badala ya kukaa ofisini ili kushughulikia changamoto za wafanyabiashara wa eneo hilo pamoja na nchi nzima kisha kumpatia ripoti kila baada ya miezi mitatu.

 

Pia amemuagiza akakae na kusikiliza wafanyabiashara hao wa Kariakoo kwa sababu ana mdomo ‘pepeta’ ambao utamaliza siasa zilizopo katika eneo hilo.

 

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Ijumaa wakati akiwaapisha viongozi wateule katika Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar.

 

Tarehe 2 Julai mwaka huu Rais Samia aliwabadilisha wizara Jafo aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kuchukua nafasi ya Dk. Ashatu Kijaji aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

 

“Kuanzia sasa pale ofisi mwenzio alipokuwa akikaa ofisini sitaki ukae, lakini namuelewa kwanini waziri (Kijaji) alikuwa haendi huko (Kariakoo),  kwa kazi ninayokupa kwa mtoto wa kike sio rahisi… kushinda Kariakoo up and down sio rahisi, hiyo kazi nataka uifanye wewe (Jafo),”  amesema Rais Samia.

 

Amemtaka akarejee ilani ya CCM inayozungumza sekta ya biashara na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukua na kustawi na kuvutia wawekezaji ili watoe mchango stahiki katika maendeleo ya nchi yetu.

 

Pia amemtaka akarejee kauli yake kwenye ufunguzi wa maonesho Sabasaba juzi aliposema serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini.

 

Amesema Kariakoo ni eneo muhimu na zuri la biashara na ndilo linaloifanya Dar es Salaam iitwe ‘commercial hub’, (mji wa kibiashara) kwa sababu mataifa yote yanakuja hapo.

 

“Lakini tumeweka pesa nyingi kujenga masoko mapya. Na masoko yakimalizika biashara pale ni saa 24. Sijui mtajipanga vipi ila ni kazi yako… Nataka pawe soko la kimaitaifa,” amesema.

Amesema Kariakoo kuna siasa kwa sababu wakati mzozo wa hivi karibuni, alituma timu kwa siri kufanya mahojiano wafanyabaishara waliopo Kariakoo na wengi wao walisema hawajui kwanini wanagoma.

 

“Ukiangalia kuna siasa. Nenda kasikilize, kaa nao pawe eneo salama la biashara. Wawe ndio rafiki zako. Nisisikie tunamtafuta waziri hatumpati hasa wewe mwenye mdomo upo pepeta. Kwa madam (Kijaji) nilikuwa namuelewa. Ndio maana nikampeleka mazingira aende akaseme na mitim” amesema.

 

Pamoja na mambo mengine amemtaka akashirikiane na taasisi nyingine ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na wizara za kisekta lakini pia pamoja na Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ili kuwapanga vizuri wamachinga.

 

“Kaa na polisi muone mnawapangaje. Kama kufunga baadhi ya barabara jioni wafanye biashara sawa,” amesema.

 

Aidha, ameonya uwepo wa wageni kufanya kazi za wazawa kama vile kuuza mtumba.

 

“Hivi karibuni nimeona Mchina anapigana na mwenyeji mwanamke, Mchina anauza mitumba, kama biashara haifai kufanywa na watu wa nje kwanini wapewe leseni,” amehoji Rais Samia.

 

Pia amemuagiza Jafo kuhakikisha wafanyabaishara wote wa eneo hilo la Kariakoo wanasajiliwa na kuwa na kanzi data madhubuti kama ilivyo kwa wamachinga kupitia taasisi yao.