Samia:Afrika ni bara la chini kuwa na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema licha ya Afrika kuwa na idadi kubwa ya watu na rasilimali zote muhimu lakini ni bara la chini kuwa na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia 

Rais Samia ameyasema hayo leo akiwa kwenye mkutano wa Kimataifa wa Nishati Safi ya kupikia kwa Afrika unaofanyika nchini Ufaransa.

Zaidi ya Waafrika milioni 900 wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia jambo ambalo linachangia uharibifu wa Mazingira, Bioanuai, na athari za kiafya.

Samia amesema yapo mambo kadhaa yanochangia Waafrika hao kuendelea kutumia nishati isiyo safi ikiwemo gharama kubwa hususani kwa watu waishio vijijini, pia ulimwengu kwa ujumla kutoweka kipaumbele kwenye suala hilo kwa kutoa ufadhili mdogo na watu kutojua fursa za kiuchumi zitokanazo na matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Aidha amebainisha kuwa iwapo dunia itaweka kipaumbele katika uwekezaji wa nishati safi ya kupikia kutawezesha wanawake kushiriki fursa nyingine za kiuchumi, kupunguza umaskini na usawa wa kijinsia.

Mkutano huo ulioanza leo umewakutanisha watu takribani 1000, wakiwemo marais, viongozi mbalimbali, watu mashughuli, asasi za kiraia, na wengine wengi.

Malengo hasa ya mkutano huo ni kuhakikisha Afrika inapata uelewa lakini pia liwe jambo la Kimataifa ambapo pia itakua rahisi kuchangia ili kuweza kutekeleza azma hiyo.

Mbali na hayo pia kuunda sera madhubuti inayotekelezeka kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na kuharakisha ushirikiano wa wadau katika suala hilo.

Inakadiriwa kuwa dola za Kimarekani bilioni 4 zinahitajika kila mwaka ili kufanikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa Waafrika wote ifikapo mwaka 2030.

Ikumbukwe kuwa Mkutano huu umeandaliwa nchini Ufaransa na Shirika la Nishati Duniani IEA