Rais Samia Suluhu Hassan amesema sifa ya Tanzania kama kisiwa cha amani imeanza kuporomoka kutokana na matukio ya vurugu, uchochezi na matumizi ya dini katika siasa, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinadhoofisha misingi iliyoiweka nchi hiyo kwenye heshima ya kimataifa kwa miongo mingi.

Akizungumza leo Desemba 2,2025, jijini Dar es Salaam katika mkutano na wazee wa jiji hilo, Rais Samia alisema hadi kufikia Oktoba 29 mwaka huu Tanzania ilikuwa ikitajwa duniani kama mfano wa amani na umoja, lakini matukio yaliyotokea baada ya siku hiyo yameanza kupunguza hadhi hiyo.
Alisema, “Kabla ya tarehe 29 Oktoba, ukitaja msamiati wa kisiwa cha amani, watu wengi walikuwa wanaitaja Tanzania. Amani, umoja na utu wetu ndivyo vilivyotutambulisha. Lakini kila siku zinavyokwenda sifa yetu inaporomoka; wengi wasioitakia mema nchi yetu wanakereka na tambo zetu.”
Akizungumzia vurugu za Oktoba 29 na 30, Rais Samia alisema hazikuwa desturi ya Watanzania na kwamba athari zake zimegusa taifa zima na hata walioshiriki wengi wao hawakuwa wanajua wanchokifanya.
“Kila aliyeumia au kupoteza maisha ni Mtanzania mwenzetu mwenye haki sawa na wengine. Hakuna sababu ya Watanzania kuumizana na kunyimana uhuru. Mtanzania mmoja akiumia, tumeumia wote,” alisema huku akitoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu.
Rais Samia alidai kuwa fujo za Oktoba 29 zilipangwa kwa makusudi na kundi la watu waliodhamiria “kuangusha dola”, akisema, “Lile lilikuwa tukio la kutengenezwa. Vurugu zile ni mradi mpana wenye nia ya ovu, wenye wafadhili, washitiri na watekelezaji. Wapo walioingia kwa mkumbo, wapo walioingia kwa tamaa, na wapo waliolipwa tu.” Amesema baadhi ya waratibu wa vurugu hizo wapo nje ya nchi na wengine ndani, na kwamba Serikali inaendelea kuwafuatilia.
Aidha, Rais Samia alishangazwa na maandamano kufanyika siku ya uchaguzi, akieleza kuwa hilo lilikuwa jaribio la kutengeneza taharuki baada ya kile alichodai kuwa wapinzani walijua wasingefanikiwa. “Kwa nini siku ya uchaguzi? Walijua kuna ushindi mkubwa wa Chama cha Mapinduzi. Hawakuzuiliwa kuingia kwenye uchaguzi; walijitoa wenyewe,” alisema.
Kuhusu tuhuma za matumizi makubwa ya nguvu na vyombo vya dola, Rais Samia alitetea hatua zilizochukuliwa, akisema, nguvu iliyotumika ilikuwa inastahili kutokana na tukio lenyewe huku akisisitiza hakuna aliye juu ya sheria hata kama unatafuta haki.“Nguvu inayotumika inaendana na tukio. Tukisemwa tulitumia nguvu kubwa..nguvu ndogo ingekuwa ipi? Tuwatazame waandamanaji waliokuwa wamejiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe? Hapo kutakuwa na dola kweli? Dola haipo hivyo.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais Samia alionya dhidi ya matumizi ya dini kuchochea chuki, akisema baadhi ya watu wanapandikiza uhasama kwa kivuli cha imani. “Hakuna eneo baya kama kumpata mtu kwenye dini. Ukimlisha ubaya unajenga chuki moyoni. Wanasiasa wanamuharibu mtu kichwani,” alisema.
Aliwataka viongozi wa dini kusimama kwenye nafasi zao na kuacha kushiriki katika misukosuko ya kisiasa, akisisitiza, “Dini zetu zinasema mamlaka yote hutoka kwa Mungu iwe mwanamke au mwanaume. Hakuna kitabu cha dini kilichoruhusu kuvuruga nchi. Viongozi wa dini, tusivuruge nchi yetu.”