Sarakasi kuelekea uchaguzi wa TLS na kuondolewa kwa Mwabukusi

Uchaguzi wa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), umekuwa na sarakasi zilizoibua wadau wa sheria nchini kufuatia kuondolewa kwa jina la miongoni mwa wagombea wa nafasi hiyo Wakili Boniface Mwabukusi jambo linalodaiwa kuwa kuna mchezo mchafu unaendelea ndani ya TLS unaoongozwa na Kamati ya Uchaguzi huo.

Mwabukusi alikuwa miongoni mwa wagombea sita waliopitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TLS kugombea nafasi hiyo Juni 24, 2024, akiwa pamoja na Ibrahim bendera (Ilala), Emmanuel Muga, (Ilala), Revocatus Kuuli (Mzizima), Paul Kaunda (Kanda ya Magharibu) na Sweetbert Nkuba (Kinondoni).

 

Ikiwa imebaki siku moja kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Kamati ya rufaa za uchaguzi ya chama hicho, ilimuengua wakili Boniface Mwabukusi kugombea urais, ikisema ana doa la kimaadili kinyume na kanuni za uchaguzi huo.

 

Mwabukusi kupinga uamuzi huo Mahakamani 

 

Baada ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kumuengua Boniface Mwabukusi katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa chama hicho, wakili huyo ametangaza kusudio la kwenda mahakamani.

 

Sambamba na hatua hiyo, amewataka wanachama wengine wa TLS kutoshiriki uchaguzi huo, ili kuishinikiza Kamati ya Uchaguzi iwarejeshe wagombea wote iliowaengua.

 

Hata hivyo, Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TLS, Nelson Frank amesema suala la kwenda mahakamani ni haki ya kila mtu na ipo kikatiba pale anapohisi hajatendewa haki au hajaridhika na uamuzi.

 

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Julai 7,2024 Mwabukusi alinukuliwa akisema safari yake tangu mwanzo wa mchakato haikuwa rahisi, kwani ilikumbwa na pingamizi nyingi, lakini kamati ya uchaguzi iliyaondoa kwa kuwa iliona hazina hoja za msingi.

 

Mwabukusi amesema hatakubali kurudi nyuma hadi haki yake ipatikane, huku akieleza atakataa ndani ya chama hicho na nje ya Mahakama kwa kuwa uchaguzi huo umekuwa wakilaghai unaenda kuendeleza mfumo wa kunyonya wanachama.

 

Amesema kwa hatua aliyofikia hatoogopa wala kutishwa na hatakata tamaa katika kupigania haki yake kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi inayoamini katika msingi wa utawala wa kisheria.

“Natakuwa Rais wa TLS, ili tuwajibike kwa wananchi hatuwezi kukaa tunalipa mamilioni ya michango kuendesha chama, halafu wahuni wachache wanavuruga kanuni zilizopo kwa maslahi yao binafsi,” amesema.

 

Mawakili na Wanarahakati wamuunga mkono 

 

Hata hivyo wadau wanasema tuhuma hizo za kimaadili dhidi ya Mwabukusi hazinamashiko badala yake uchaguzi huo unawafanya kuwa na maswali mengi yasiyo na majibu.

Kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter, Wakili Peter Kibatala, ataendelea kupinga mchakato wa uchaguzi na kususia mikutano akieleza kuwa chama hicho ndio ukuta wa mwisho wa kuulinda umma.

“Nitashiriki kuwashawishi wengine wafanye hivyo, kwa wakati huu nitashirikiana na wakili Mwabukusi katika kusaka haki yake ya kisheria. Kwa hali ilivyo, sioni kuna uchaguzi halali ndani ya TLS,” alisema Kibatala.

Mmoja wa wagombea urais, Kapteni Ibrahim Bendera, alisema uamuzi wa Mwabukusi kwenda mahakamani ni sahihi kwa kuwa ni chombo cha kutoa haki.

“Hatuwezi kulazimisha kamati imrejeshe, lakini naamini mahakamani atapata haki stahiki. Mwenyewe keshasema atakata rufaa, tusubiri maamuzi ya mahakama na matokeo ya rufaa,” alisema.

Kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya wanaharakati wameunga mkono uamuzi wa Mwabukusi kushinikiza arejeshwe kuwania nafasi hiyo, wakieleza kuwa ana haki kisheria na kikanuni.

Lakini pia wengine wamekwenda mbali zaidi kwa kuishutumu TLS kuwapitisha wagombea ambao wengine ni wateule wa Rais ambao miongoni mwao akiwa amefukuzwa kazi kwa matumizi mabaya ya fedha.

Kwa miaka mingi, uchaguzi wa TLS umekuwa ukivuta hisia za wananchi ndani na nje ya chama hicho, huku sarakasi zikitawala.

Mwaka 2016, Seka alienguliwa na baada ya mawakili ‘kuijia juu’ kamati ya uchaguzi, ilimrejesha na akachaguliwa kuongoza chama hicho.

Uchaguzi wa TLS umekuwa wa mchakamchaka kutokana na majukumu yake ambayo ni pamoja na kuishauri serikali na taasisi zake.

TLS ilianzishwa kwa sheria mwaka 1954 kama chama cha kitaaluma cha mawakili nchini na kifungu cha 4 cha sheria hiyo (Sheria ya Chama cha Mawakili wa Tanganyika), inabainisha majukumu makuu matatu ya taasisi hiyo.

Moja ya jukumu hilo ni kuwaunganisha, kuwatetea na kusaidia ustawi wa mawakili nchini.

Pili, kuishauri Serikali na vyombo vyake kama Bunge na Mahakama. Jukumu jingine ni kusimamia maslahi na ustawi wa jamii ya Watanzania.

Jukumu jingine ni kusimamia maslahi na ustawi wa jamii ya Watanzania.

Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 2, 2024, jijini Dodoma utakaokwenda sambamba na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa TLS.