Serengeti Girls yapewa heshima ya pekee ndani ya bunge la Tanzania

Timu ya soka ya Taifa ya wasichana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Girls’, leo imepewa heshima kubwa kwa kuingia ndani ya ukumbi wa bunge la Tanzania mjini Dodoma.

Wachezaji wa timu hiyo na baadhi ya maofisa, walipewa heshima hiyo kwa kuingia ndani ya ukumbi wa bunge, huku wakipigiwa makofi na wabunge.

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliwapongeza wachezaji hao kwa heshima waliypoewa kukalia viti vya bungeni na kuagiza wakafanye kweli katika Kombe la Dunia huko India Oktoba mwaka huu.

Serengeti Girls imefuzu fainali za Kombe la Dunia kwa kuitoa Cameroon kwa jumla ya mabao 5-1.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake mara baada ya kupewa fursa na Spika Tulia, nahodha wa timu hiyo, Noela Patrick, amesema watawapa raha Watanzania kwa kufanya vizuri katika fainali za Kombe la Dunia nchini India Oktoba mwaka huu.

“Rais Samia anaupiga mwingi hapa nchini… sisi tunamuahidi tutaupiga mwingi India,” amesema Noela na kuongeza kuwa wanashukuru ahadi ya kwanza waliyomuahidi Rais Samia ya kufuzu fainali hizo wameitekeleza.

Serengeti Girls imekuwa timu ya kwanza kukaa eneo maalum wanalokaa wabunge kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Timu hiyo imealikwa bungeni baada ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia litakalofanyika India Oktoba mwaka huu.

Aidha Dk. Tulia Ackson ameagiza timu ya soka ya Taifa ya watu wenye ulemavu ‘Tembo Warriors’, ipelekwe bungeni kesho kupongezwa kwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia.

Spika alisema kwa vile Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa, amesema Tembo Warriors imefuzu fainali za Kombe la Dunia, hivyo nayo ipelekwe bungeni.

“Naagiza Tembo Warriors nao waletwe bungeni kesho,” amesema Spika Tulia na kushangiliwa na wabunge.