Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Dkt. Damas Ndumbaro amesema Serikali imezingatia vyema suala la Haki za Binadamu kwa wakazi waliokuwa wanaishi Ngorongoro kisha kuamua kuanza kuondoka kwa hiyari yao kuelekea Kijiji Cha Msomera wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.
Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo kwenye kikao na wadau wa Haki za Binadamu, Mawaziri pamoja na Wakuu wa Mikoa ya Arusha na Tanga, nchini humo kilichofanyika June 21,2022.
Waziri Ndumbaro alisema imekuwa ni muhimu wadau wa Haki za Binadamu kukutana na kujadili suala la Ngorongoro na Loliondo ili kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa na kujibu hoja zisizo za kweli zinazosambaa kwa haraka katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
“Serikali imezingatia vyema haki za binadamu, imewajengea nyumba wananchi walioamua kuhama kwa hiyari, imewapa maeneo yasiyopungua hekari 3 kila mmoja, imewasafirisha wao na mizigo yao na mifugo wanayomiliki, lakini pia Serikali imewalipa fidia, “. amesema Dkt.Ndumbaro
Awali, Dkt. Ndumbaro alitoa wasilisho katika kikao na Mabalozi kutoka nchi mbalimbali na taasisi za kimataifa, liloonesha jinsi Serikali inavyozingatia haki na malengo yake kuboresha hali ya watanzania wa maeneo ya Ngorongoro na Loliondo.
Waziri Ndumbaro alisema kwa upande wa Loliondo, Serikali imewapa wananchi zaidi ya asilimia 62 ya eneo la hifadhi ya Loliondo ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa sasa na imebakiwa na kiasi cha Kilomita za mraba 1500 kutoka 4000 za awali.
Amesema kinachoendelea katika eneo la Ngorongoro kwa wakati huu ni uhamaji wa hiari wa wananchi waliokuwa ndani ya eneo la Ngorongoro na sio kwamba kuna uhamishaji wa nguvu unaofanywa na Serikali.
“Serikali imekuja na mpango wa kulinda eneo la Ngorongoro, imechukua miaka 20 kuandaa na kuratibu mpango huu, ambao unatekelezwa sasa na hakuna uhamishaji wa nguvu unaofanywa kwa wananchi kama inavyodaiwa, wananchi husika wameshirikishwa vya kutosha na ndio maana wamekubali na kuamua kuhama kwa hiari wenyewe,” alisema Dkt. Ndumbaro.
Amesema Katiba ya Tanzania inasema watu wote ni sawa na kila mtu ana haki ya kuishi popote na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu wananchi wake wote bila ya kujali rangi, kabila au dini zao.
Ameeleza kuwa wananchi wamepewa umiliki kwa miaka kadhaa na endapo itaonekana kuna haja ya kuichaukua ardhi hiyo anayeimiliki hulipwa fidia na kupewa ardhi katika eneo lingine na kuongeza kuwa wananchi wanaohama kwa hiari yao kutoka katika hifadhi ya Ngorongoro wanalipwa fidia na kupatiwa nyumba za makazi, maeneo yenye huduma za kijamii na ardhi kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema kuwa Serikali imechukua jukumu la kukata eneo la Loliondo SQM 4000 ambazo zina usajili na eneo la SQM 2500 likakatwa kwa ajili ya matumizi ya Wananchi.
Amesema kuwa vyombo vya Habari vimekuwa vikipotosha kuhusu eneo hilo kwa kutaka kuharibu taswira ya wawekezaji nchini Jambo ambalo halina manufaa kwa Taifa.
” Vyombo vya Habari vinapotosha kuhusu mwekezaji aliyepo zaidi ya miaka 30 ambapo kila mwaka vitalu vya eneo Hilo hutangazwa kisheria na kuingizwa katika minada ambapo mwekezaji huyo huibuka mahindi na kupata eneo lake kisheria”, alisema Masanja
Aidha kwa upande wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia amehudhuria mkutano huo Balozi Liberata Mulamula ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa nchini kuwa inazingatia na kutekeleza sheria za kimataifa za haki za binadamu huku ikiendelea kulinda uhifadhi wa eneo la Ngorongoro.
“Napenda kuchukua nafasi hii kuuhakikishia umma wa Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuwa Tanzania inazingatia na kutekeleza sheria za kimataifa za haki za binadamu na hakuna nanma itaendesha mipango yake kwa kukiuka sheria za haki za binadamu”, alisema Balozi Mulamula.
Balozi Mulamula ameongeza kuwa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inatekeleza mpango wa kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro nchini kwa wananchi kuridhia kuhama kwa hiari yao na kwamba hakuna aliyeondolewa katika eneo hilo kwa nguvu kama inavyoelezwa.
“Tanzania siku zote italinda watu wake, maliasili zake na mipaka yake kwa kuzingatia sheria za kimataifa,” alisema Balozi Mulamula.
Mkutano huo uliohusisha viongozi waandamizi wa Serikali kutoka Wizara za mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Maliasili na Utalii, Katiba na Sheria pamoja na Wakuu wa Mikoa ya Arusha na Tanga.
Mkutano huo ulilenga kuwafahamisha wanadiplomasia walioko nchini juu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuhama kwa hiari kunakofanywa na wananchi waliokuwa na makazi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na hivyo kuondoa sintofahamu iliyokuwepo kuwa wananchi hao wanahamishwa kwa nguvu na serikali na hivyo kukiuka haki za binadamu.