Serikali ya Tanzania inatarajia kukusanya na kutumia shilingi trilioni 44.38 kwa mwaka 2023/2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.0 ya bajeti ya mwaka 2022/2023.
Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania Dk Mwigulu Nchemba ameyasema hayo leo wakati akiwasilisha kwa wabunge mapendekezo ya mpango wa Maendeleo wa Taifa na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka 2023/2024.
Bunge mwaka jana lilipitisha shilingi trilioni 41.48 kwa ajili ya bajeti ya mwaka 2022/2023 kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka huo wa fedha.
Amesema katika mwaka wa 2023/2024 mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa ni shilingi trilioni 31.38 sawa na asilimia 70.7 ya bajeti yote.
“Kati ya mapato hayo, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 13.0 hadi Sh26.72 trilioni kutoka makadirio ya shilingi trilioni 23.65 mwaka 2022/23,”amesema.
Amesema misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo inatarajiwa kufikia shilingi trilioni 5.46 sawa na asilimia 12.3 ya bajeti yote.
Aidha, Dk Mwigulu amesema Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 5.44 kutoka soko la ndani ambapo shilingi trilioni 3.54 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva.
Amesema pia shilingi trilioni 1.89 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na kwamba Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 2.1 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu.