Waziri wa Maendeeo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum nchini Tanzania Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali ya nchi hiyo kupitia Wizara za Kisekta imeanza mapitio ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 pamoja na sheria nyingine zinazogongana ili kuwasaidia watoto wa kike kuhusu umri wa kuolewa.
Wazir Gwajima ametoa kauli hiyo jana wakati akishiriki mjadala katika Jukwaa la Msichana “Girl Ajenda Forum 2022” lililoandaliwa na Wadau mbalimbali kwa lengo la kusikiliza Masuala yanayowahusu wasichana ikiwa leo dunia inaadhimisha siku ya Kimataifa ya Mtoto wa kike ambayo hufanyika kila mwaka Oktoba 11.
Katika Jukwaa hilo mambo yaliyojitokeza ni pamoja na suala la mkanganyiko wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 na sheria ya Mtoto (1999) hususani kuhusu umri wa kuolewa.
“Suala la sheria ya ndoa limeanza kufanyiwa kazi na Kamati maalum kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, hatua iliyopo ni kukusanya maoni ya wananchi ili kuwa maamuzi ya pamoja kama Taifa” amesema Gwajima.
Suala lingine ni gharama ya taulo za kike ambapo wasichana wameiomba Serikali kupunguza tozo kwa taulo hizo au kuondolewa kabisa kwa sababu wengi wao hasa maeneo ya vijijini wanashindwa kumudu gharama hizo hivyo kushindwa kuhudhuria masomo wakiwa katika siku za hedhi.
Waziri Gwajima amesema kuhusu suala la tozo kwenye taulo za kike amelipokea, ataliwasilisha kwenye Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ina dhamana ya tozo ili itoe maelekezo, na pia amebainisha ipo haja ya kuwa na viwanda vya taulo za kike ndani ya nchi na ni fursa kwa wawekezaji wa ndani na wanawake hasa kupitia mabaraza ya uwezeshaji Wanawake kiuchumi.
Wakichangia mada katika jukwaa hilo Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Taifa Nancy na mwakilishi wa watoto Liku wamesema watoto wengi wa kike wanakosa fursa ya kuhudhuria masomo wakiwa katika hedhi hivyo kuchangia kudondoka kimasomo.
“Tunaiomba Serikali yetu iweze kuliangalia suala la kodi katika taulo za kujisitiri” amesea Liku, mwanafunzi wa kidato cha tano shule ya sekondari Tinde.
Naye Mkurugenzi mkuu wa shirika la Kimataifa linaloshughukia masuala ya wanawake (UNWOMEN) Ms Sima Sami Bahous amesema watahakikisha changamoto walizozianisha zinafanyiwa kazi.