Serikali ya Tanzania yakanusha ukandamizaji wa kisiasa wakati uchaguzi ukiakaribia

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekanusha madai yanayodai ongezeko la ukandamizaji wa kisiasa nchini humo, huku taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akijibu ripoti iliyotolewa na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu, Human Rights Watch (HRW), Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema madai hayo hayana msingi na yanapotosha hali halisi ya nchi.

“Madai kwamba uhuru wa kisiasa umepungua kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 siyo ya kweli,” amesema Msigwa. Amesisitiza kwamba katiba ya Tanzania inatoa haki ya kuishi, usalama na uhuru kwa kila Mtanzania.

Aidha, Msemaji huyo amepuuzilia mbali madai ya taarifa za kutekwa kwa raia nchini humo na kulaumu shirika la HRW kwa kutoa ripoti hiyo bila kuipa serikali fursa ya kujibu. Hata hivyo, amesema serikali ipo tayari kushirikiana na taasisi yoyote inayohitaji taarifa sahihi.

Kwa mujibu wa ripoti ya HRW, Serikali  ya Tanzania imedaiwa kukandamiza upinzani, kunyamazisha vyombo vya habari na kushindwa kuhakikisha uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Ripoti hiyo pia inatoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua za haraka kulinda uadilifu wa uchaguzi mkuu, ambao shirika hilo linasema uko katika hatari.

Nomathamsanqa Masiko-Mpaka, mtafiti wa Afrika katika HRW, amesema:
“Mamlaka inahitajika kujizuia kukandamiza upinzani na vyombo vya habari, na badala yake kushiriki katika mageuzi yenye maana ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.”

Serikali ya Tanzania imefafanua kwamba imejipanga kuhakikisha haki za binadamu, demokrasia, utawala bora na heshima ya sheria vinazingatiwa kabla, wakati, na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.