Serikali ya Tanzania yataja vipaumbele mpango wa maendeleo 2024/25

Serikali imewasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2024/25. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo aliwasilisha mpango huo Dodoma jana katika kikao cha kamati ya bunge zima kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Profesa Kitila alisema mpango huo unalenga kuendelea kuchochea kasi ya ukuaji uchumi ambao ni jumuishi, unaopunguza umaskini na kuleta ustawi kwa wote, unaozalisha ajira kwa wingi na unaochochea mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi. 

Aliwaeleza wabunge kuwa msukumo utawekwa katika kuongeza tija ya uzalishaji na uongezaji wa thamani wa mazao katika sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, misitu na madini.

Pia Profesa Kitila alisema mpango huo unalenga kuchochea na kuboresha ubora wa elimu na mafunzo katika ngazi zote, kuongeza na kuimarisha matumizi zaidi ya teknolojia hasa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

Alisema pia unalenga kuongeza uzalishaji viwandani na kuimarisha huduma bora za jamii kwa wote zikiwemo za afya na upatikanaji wa maji safi na salama kwa wote. Wabunge walielezwa kipaumbele kitawekwa katika kukamilisha programu na miradi ya maendeleo inayoendelea hususani miradi ambayo ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.

Aidha, Profesa Kitila alisema miradi mipya itakayotekelezwa katika mwaka 2024/25 ni itakayoongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, kutoa matokeo ya muda mfupi, kupunguza umasikini na kuongeza mapato ya serikali hususani fedha za kigeni.