Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Serikali ya Tanzania yatarajia kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi trilioni 43. 29 kwa mwaka wa fedha 2023/24 - Mwanzo TV

Serikali ya Tanzania yatarajia kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi trilioni 43. 29 kwa mwaka wa fedha 2023/24

Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Mwigulu Nchemba amewasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka wa fedha 2023/24 katika Kamati ya Bunge zima ambapo inatarajia kukusanya na kutumia shilingi trilioni 43.3.

Dk Mwigulu amesema Serikali ya Tanzania katika mwaka 2023/24, inatarajia kukusanya na kutumia shilingi trilioni 43.3 ikilinganishwa na makadirio ya shilingi trilioni 41.5 kwa mwaka 2022/23, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.4.

Mapendekezo hayo amewasilisha leo Novemba 7, 2022 bungeni jijini Dodoma ikiwa ni Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/24 katika Kamati ya Bunge zima.

Dk Mwigulu amesema ongezeko hilo limezingatia mwenendo halisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na jitahada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuongeza mapato.

Aidha, amesema ongezeko hilo limezingatia mahitaji yasiyoepukika kama vile mikataba ya kugharamia miradi mbalimbali, deni la Serikali na mishahara ya watumishi wa umma.

Amesema mwaka 2023/24, mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 31.03, sawa na asilimia 71.7 ya bajeti yote.

Aidha, amesema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi trlioni 4.51 sawa na asilimia 10.9 ya bajeti.

Amesema pia Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 5.63 kutoka soko la ndani ambazo zinajumuisha shilingi trilioni 3.54 kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na shilingi bilioni 2.09 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Amesema mikopo ya masharti ya kibiashara kutoka nje inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 2.11.

“Baadhi ya mikakati itakayotumika katika kufikia lengo la makusanyo ya mapato ya ndani ni pamoja na kuendelea kuwatengea wafanyabiashara na watoa huduma wadogo maeneo maalum kwa lengo la kukuza biashara zao,” amesema.

Dk Mwigulu amesema mikakati mingine kutambua na kusajili kampuni za kimataifa zinazoendesha biashara za kidigitali nchini kwa kutumia mfumo wa usajili uliorahisishwa na kuwekeza kwenye matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha mifumo ya Serikali inabadilishana taarifa.

Mingine ni kusimamia mikakati ya kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya wizara na idara zinazojitegemea na kuimarisha hatua za kiutawala za usimamizi na ukusanyaji wa kodi.