Serikali ya Tanzania yawachinjia nyama Wahadzabe ili washiriki zoezi la Sensa   

Jamii  ya Wahadzabe wilayani Karatu, mkoani Arusha nchini Tanzania, wamechinjiwa pundamilia pamoja na nyumbu, ili wawepo kwenye makazi yao wakati makarani wa sensa ya watu na makazi watakapopita kuwahesabu.

Akizungumza mjini Karatu, wakati Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, amesema waliamua kuwachinjia jamii ya Wahadzabe, pundamilia wawili na nyumbu wawili, pamoja na kuwapa ndizi mbivu, ili wawepo katika makazi yao kwa ajili ya kuhesabiwa.

“Wahadzabe chakula chao kikuu ni nyama za kuwinda pamoja na matunda, sisi tumeona tuwapatie chakula, ili tuweze kuwapata na kuwahesabu na zoezi letu limefanikiwa.

“Hili ni kundi maalumu, sababu wao ni wawindaji, hivyo tumeweza kuwahesabu kutokana na kukidhi mahitaji yao kupitia kwa viongozi wao na  tumewahesabu vizuri,” amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa Sensa Wilaya ya Karatu, Rose Mipango amesema zoezi la sensa limeenda vizuri.

Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi nchini Tanzania limeanza hapo jana Agosti 23,2022 ikiwa ni sensa ya sita nchini humo ambapo sensa ya mwisho ilifanyika mwaka 2012.

Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.