Search
Close this search box.
Africa

Serikali ya Zanzibar imesema itafidia gharama za chakula na mafuta  zilizochangiwa na vita vya Urusi 

11
Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi

Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi amesema serikali yake imeamua kufidia gharama za mafuta na chakula, ambazo zimechangiwa na mgogoro wa vita kati ya Urusi na Ukraine, pamoja na maamuzi ya hivi karibuni ya China kuzuia watu kutoka nje.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 31. Ikulu Zanzibar, Rais Mwinyi alieleza kuwa mgogoro wa Ukraine umechangia kwa kiasi kikubwa kuyumba kwa uchumi wa dunia, ikiwa ni pamoja na kuongeza gharama ya mafuta na usafirishaji.

“Ukraine ni mzalishaji mkubwa wa ngano. Hivi tunavyozungumza ngano imepanda bei. India wamezuia usafirishaji kutoka nje ya nchi na sasa Indonesia na Uturuki pia zimezuia usafirishaji wa mafuta ya kula,” amesema Rais Mwinyi.

Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, serikali ya Zanzibar inatoa shilingi bilioni 3 kila mwezi kupunguza ongezeko katika bei ya mafuta ya petroli, dizeli na yale ya taa.

Pia imepunguza ushuru wa kuingiza mazao ya chakula na kulazimika kuweka bei elekezi, ili kusaidia kukabiliana na ongezeko la bidhaa hizo.

Amesema haijulikani utaratibu huo utaendelea kwa muda gani.

“Inategemea uwezo wa serikali, na pengine inategemea tatizo litachukua muda gani,” amesema.

Katika hatua nyingine Rais Mwinyi ametoa wito kwa wafanyabiashara kulipa kodi kwa uaminifu, huku akiwataka wananchi kudai risiti ya EFD pale anaponunua bidhaa.

“Mambo haya Serikari inafanya kukabiliana na hali ngumu ya maisha yanapelekea kupunguza ushuru kwa kiwango kikubwa, tunatoa fedha za serikali kufidia, hivyo ni lazima tukusanye kodi zilizobaki kwa umakini mkubwa.

“Mashine za EFD  wafanyabiashara hawatumii, wananchi kila unachonunua dai risiti, bila hivyo serikali itashindwa kufanya haya inayofanya.

“Ukienda darajani ukinunua kitu utasikia ‘system’ ipo chini, wanafanya makusudi wafanyabiashara, wito wangu mamlaka husika ichukue hatua zinazostahili, serikali inabeba gharama kubwa kufidia huku hatukusanyi ushuru itakuwa ni mzigo mkubwa  sana,” amesema Rais Mwinyi.

Comments are closed

Related Posts