Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, amesema kwa sasa nguvu kubwa imeelekezwa katika mikoa sita korofi kwa matukio ya ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha kasi ya matukio hayo inapungua.
Mikoa inayoongoza kwa matukio ya ukatili ikiwamo vipigo, mauaji, ubakaji imetajwa kuwa ni Mara, Manyara, Dodoma na Singida.
Hayo yamesemwa leo ikiwa ni katika kuelekea siku ya wanawake duniani inayoadhimshwa kila mwaka Machi 8.
“Mikoa inayoongoza kwa ukatili ni pamoja na Mara, mkoa wa Manyara, Dodoma na Singida pia ipo mingine miwili kwa sasa nguvu kubwa tumeelekeza huko tukiona imeanza kupunguza kasi tutasema tumefanikiwa kupunguza ukatili” amesema Waziri Gwajima
Ameongeza kuwa “Katika kuelekea kilele cha maadhimisho kuanzia leo kutakua na vipindi mbalimbali na mada za ukatili zitakua ndani yake. Mwezi wote wa Machi tumejipanga suala la ukatili tutalijadili kupambana na ukatili wa kijinsia mwarobaini wake ni jamii yenyewe,”
Aidha Dk Gwajima amesema suala la ukatili ni la kijamii na litamalizwa na jamii yenyewe, hivyo kinachotakiwa ni matokeo na siyo lazima kufuata mwongozo ulivyo katika utendaji
Amesema viongozi mbalimbali wa kitaifa wataungana na mikoa mbalimbali kuadhimisha kwa uratibu wa mikoa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu itashiriki maadhimisho haya mkoani Arusha.