SHAHIDI ADAI KUVULIWA NGUO NA KUNING’INIZWA KWENYE BOMBA

Walinzi wa Mbowe (Aliyekati, Adam Hassan Kasekwa)

Shahidi wa kwanza katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayowakabili Freeman Mbowe na wenzake watatu Adam Kasekwa,ameileza mahakama kuwa wakati akiwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi alipata mateso ikiwemo kuchomwa bisibisi katika maeneo ya kwenye mbavu na makalioni.

Ushahidi huo ameutoa leo mbele ya Jaji Mustapha Siyani ikiwa ni baada ya upande wa Jamhuri kuileza Mahakama kuwa wamefunga ushahidi wao kwa mashahidi watatu kati ya mashahidi saba waliopanga hapo awali kuwaleta.

Shahidi ambaye ni mshtakiwa namba mbili kwenye kesi ya Uhujumu Uchumi ambayo ndani yake kuna makosa ya Ugaidi akiongozwa na mawakili wa utetezi John Malya , Peter Kibatala na Nashon Nkungu ameiambia Mahakama kuwa alipata mateso karibu muda wote aliokua chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi. Ikumbukwe kuwa mbali na shahidi huyo ambaye ni mshtakiwa anayejitetea mwenyewe mawakili wa utetezi wamepanga kuleta mashahidi wengine watatu.

Shahidi huyo ameiambia mahakama kuwa mara ya kwanza alipokamatwa alikuwa mjini Moshi ambapo alikua huko kwa ajili ya kukutana na Freeman Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa CHADEMA lengo likiwa ni kuweka makubaliano ya mkataba wa kufanya kazi ya ulinzi aliyoombwa na Mbowe.Shahidi anaeleza kwamba akiwa maeneo ya Rahu Madukani ambapo alikua akipata chakula na mwenzake ambaye ni mshtakiwa namba tatu Mohamed Ling’wenya walishangaa kuona wanavamiwa na kikundi cha watu watano ambao walimchukua shahidi huyo na kuanza kumpiga.

Mwenzake ambaye ni Mohamed Ling’wenya alipooona sintofahamu hiyo alikwenda kuwauliza watu hao kwanini wanampiga mwenzake ndipo wakachukua silaha na dawa za kulevya walizokuwa nazo wakamuwekea.Amesema Adam Kasekwa shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi.

Kwa mujibu wa shahidi huyo tukio hilo limetokea tarehe 5 Agosti 2020, mjini Moshi ambapo ameileza mahakama kuwa baada ya kukamatwa na kuwekewa silaha aina ya bastola na dawa hizo za kulevya amesema amemsikia mmoja ya waliomkamata akiwaambia wenzake kua wamemkuta na dawa za kulevya pamoja na silaha hiyo kitu ambacho si kweli.

Katika ushahidi wake shahidi ameiambia mahakama kua baada ya kuambiwa hivyo amri ilitolewa kupelekwa kituo cha polisi Moshi na walipofikishwa huko shahidi huyo amedai kuwa aliteswa pia akiwa ndani ya kituo hicho kwa kuvuliwa nguo zote na kisha kumfunga miguu na kumning’iniza kwa bomba mithili ya mishikaki.Shahidi ameileza mahakama kuwa muda wote alikua akipigwa kwa takribani dakika 30 hadi 45 kiasi ambacho alipoachiwa alishindwa kutembea. Akiwa ndani ya kituo hicho majira ya jioni aliona askari mmoja ambaye hakumfahamu jina lake aliona akimwaga maji ndani mahabusu aliyokuwa yeye.

Akiendelea kutoa ushahidi huo Adam Kasekwa ameileza mahakama kuwa usiku wa tarehe  6 Agosti, alitolewa ndani ya kituo hicho cha polisi Moshi na kufungwa macho kwa kutumia jaketi pasipokujua anapelekwa wapi.Shahidi  ameendelea kuileza mahakama kuwa ilipofika tarehe 7 alijikuta amefikishwa katika kituo cha Polisi Tazara jijini Dar es Salaam na sababu ya yeye kujua kuwa yupo kituo cha Tazara ilikua ni baada ya kuwauliza watuhumiwa wengine aliowakuta ndani ya kituo hicho.

Ilipofika tarehe 9 Agosti 2020 usiku alifungwa tena uso na kisha kuchukuliwa usiku huo na kupelekwa sehemu nyingine ambapo alikuja kugundua baadae kuwa alikua katika kituo cha Polisi Mbweni, ambapo huko alikutana na shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri Afande Ramadhani Kingai aliyemtaka kusaini karatasi ambazo hakujua maelezo yake yanahusu nini.

Adam Kasekwa amewahi kutumikia Jeshi la Wananchi Tanzania kwenye kikosi cha makomandoo cha KJ, kilichoko Sangasanga mkoani Morogoro, kwa takribani miaka 6.Aliachishwa kazi na wakuu wake wa kazi kutokana na sababu za kiafya zilizogundulika baada ya yeye kutoka kwenye mapigano ya ulinzi wa amani aliyokwenda kuyafanya huko nchini Congo.Kesi inaendelea.