Shahidi akana kuona mpango wa Mbowe kupanga njama za Ugaidi

Shahidi wa kumi katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu amesema hakuna mahali katika mawasiliano ya simu zote nne alizopelekewa ofisini kwake ambapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ametajwa.

Shahidi huyo wa upande wa Jamhuri Inspekta wa Polisi Innocent Ndowo, ametoa ushahidi wake huo jana  katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Katika mahojiano yake na Wakili wa utetezi Peter Kibatala hakuweka wazi iwapo katika uchunguzi wa mawasiliano ya simu alioufanya kuna ujumbe wenye viashiria vya moja kwa moja vya mpango wa kutekeleza makosa ya ugaidi.

Ndowo ambaye ni mchunguzi wa kisayansi mwenye uwezo wa kuingilia mawasiliano ya simu, alieleza alichokiona alipokuwa akihojiwa na kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala.

Akijibu maswali ya Dodoso kutoka kwa Wakili huyo shahidi alidai kuwa alichokitoa kwenye ripoti yake ndicho alichokikuta kwenye mawasiliano hayo.

Ndowo alisema, Julai 2021 alifanya uchunguzi wa mawasiliano baina ya Mbowe na Dennis Urio ya njia ya Telegram, WhatsApp, meseji ‘sms’ katika simu nane alizopelekewa na simu nne zilionesha matokeo chanya huku nne hazikuonesha.

Kwa mujibu wa Ndowo, Mbowe anadaiwa kuwasiliana na Denis Urio, anayedaiwa kumpa kazi ya kuwatafuta waliokuwa makomandoo hao wa JWTZ kwa lengo la kupanga njama za ugaidi.

Alipoulizwa kama kuna mahali mawasiliano hayo yalimtaja Sabaya au kupanga kufanya ugaidi Ndowo alidai kuwa barua aliyopokea haikumwelekeza kutafuta taarifa hizo lakini baadaye Kibatala alipotaka kujua iwapo angekaa kimya kama angekuta taarifa za aina hiyo alisema asingeweza kukaa kimya na angeandika kwenye ripoti yake.

Shahidi huyo pia alikaa kimya pale alipoulizwa kama katika mawasiliano hayo kuna mahali alikuta watu wakipanga kulipua madaraja.

Alipoulizwa uwepo wa mawasiliano yoyote yanayozungumzia bunduki aina ya A5340 Luger, Ndowo alimwambia Jaji kuwa Kibatala alikuwa akimuuliza mambo ambayo hakuyafanyia kazi lakini pia alikiri kuwa hakuna mahali miamala ya fedha aliyoiona katika mawasiliano hayo imeeleza kuwa ni kwa ajili ya kutekeleza vitendo vya ugaidi.

Pia shahidi huyo alishindwa kuleza ni kwa namna gani aliruhusu vielelezo kuchukuliwa na mtu ambaye siye aliyevipeleka pamoja na kwamba aliileza mahakama kuwa mtu anayepeleka vielelezo ndiye anayepaswa kuvichukua tena kwa kuweka saini katika kitabu maalumu.

Kwa mujibu wa Ndowo vielelezo hivyo vilipelekwa kwake na afande Goodluck wakati aliyevichukua alikuwa ni afande Swila.

Aidha Ndowo alikana madai ya kuwepo kwa kikundi ndani ya jeshi la Polisi ambacho kilihusika na kupanga njama za kumpa Freeman Mbowe kesi ya ugaidi kama ambavyo Wakili Kibatala alidai.

Haya ni baadhi ya Mahojiano ya Wakili Peter Kibatala na Shahidi hapo jana katika Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi.

Kibatala: Kwa mujibu wa barua iliyotoka ofisi ya DCI ambayo haipo, hizo namba na simu zinachunguzwa kwa tuhuma za ugaidi?

Shahidi: Nimeona kosa limeandikwa pale

Kibatala: Mwambie Jaji tuhuma za ugaidi ni subject ya uchunguzi wako?

Shahidi: Barua ile imetaja jalada namba na kosa la tuhuma za ugaidi

Kibatala: Ulifanya basic detective course kama train? Ulifanya mafunzo yote ya kijeshi ikiwemo upelelezi?

Shahidi: Ni yapi? Mengine siwezi kueleza

Kibatala: Sehemu ya mafunzo ni upelelezi au la?

Shahidi: Baadhi ya watu wanafundishwa upelelezi

Kibatala: Wewe? Ulifundishwa basics za upelelezi?

Shahidi: Nilisoma basics za upelelezi

Kibatala: Barua inasema kosa la kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi, achana na terms of reference (hadidu rejea) mwambie Jaji katika  uchunguzi wako wa vifaa, kwa mujibu wako unaweza chunguza kosa ukaona kosa A na kosa B?

Mwambie jaji kipi uliona kinakupa kiashiria watu walipanga njama za vitendo vya ugaidi?

Shahidi: Swali hilo anapaswa kujibu mpelelezi

Kibatala: Nasema wewe

Shahidi: Mimi nilifanya analysis, mimi sikujua kitu gani kinahusisha tuhuma za ugaidi

Kibatala: Extraction (unyonyaji taarifa kutoka katika simu) yako Iliona kiashiria chochote cha watu kupanga njama  za ugaidi?

Shahidi: Nilichokiona ndicho nilichokitoa

Kibatala: Katika uchunguzi wako ukiacha term of reference, uliona mawasiliano ya watu wanapanga au wanamtaja Sabaya?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji,  katika terms of reference haikumtaja Sabaya, record ingeelekeza kumtafuta Sabaya ningechunguza

Kibatala: Ni wewe ama sio wewe dakika chache zilizopita ulisema unaweza ukapata reference kuhusu kosa A, ukaona na B?

Shahidi: Nilisema unaweza kuta vitu vingine, issue zingine ukaunganisha pamoja na hiyo issue

Kibatala: Hivyo vitu ulivyoviona kuna mahala uliona mawasiliano kutoka hizo simu nane, watu wakipanga kufanya chochote cha kumdhuru Sabaya?

Shahidi: Sikuelekezwa kufanya uchunguzi kuhusu Sabaya. Ningekuwa nimeombwa kutafuta ningefanya,  lakini sikuombwa kutafuta

Kibatala: Tukiachana na  terms of reference kuhusu Sabaya, umeona kuhusu watu kulipua madaraja katika ushahidi wako wote uliowahi ona. Umesema  chochote kinachohusiana na watu kupanga njama za ugaidi?

Shahidi: Nilichokiona ndicho nilichokitoa mahakakani

Kibatala: Wakati unafanya extraction  kuna mahala popote uliona mawasiliano ambayo yanaonesha watu wamefanya maandamano nchi nzima?

Shahidi: Sikuelekezwa kufanya uchunguzi huo

Kibatala: Uliona mahala popote watu wakizungumza chochote kuhusu kupeana, kuiba au kununua bunduki aina ya Rugger A 5340?

Shahidi: Naomba urudie

Kibatala: Katika process yote uliwahi ona mawasiliano, yawe Telegram ambayo watu wenye navyo wakizungumzia bunduki yenye usajili namba A5340 aina ya Rugger?

Shahidi: Unaongea kitu ambacho sikufanyia kazi, sikuombwa kutafuta hiko kitu

Kibatala: Kuna sms Telegram  au WhatsApp inaonesha nimetuma fedha kwa ajili ya kufanya ugaidi?

Shahidi: Nakumbuka text katika  Telegram kuna mawasiliano ya fedha

Kibatala: Nitafutie sehemu ambayo meseji ambazo  umezi-extract inasema  kwamba fedha hizi ni kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, iko meseji?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji naomba ajikite kwenye taarifa nilizofanyia kazi, kilichopo pale ndicho nilichokifanya

Kibatala: Kwa uchunguzi wako wewe ungekuta taarifa za kupanga uhalifu ungeacha kuandika kwenye riport yako kwa sababu hujaambiwa kwenye _terms of reference?_

Shahidi: Mimi ni askari polisi, kama ningekuta meseji za kupanga uhalifu ningeweka kwenye ripoti yangu.

Katika kesi hiyo, Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita ya ugaidi, ikiwemo la kukutwa na silaha aina ya Rugger, kukutwa na sare na vifaa vya JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Pia wanadaiwa kushiriki vikao vya kupanga njama za ugaidi, kutoa fedha zaidi ya shilingi 600,000 kwa ajili ya kufadhili vitendo hivyo na kupanga kulipua vituo vya mafuta na maeneo yenye mikusanyiko ya watu, pamoja na kupanga njama ya kuwadhuru viongozi wa Serikali akiwemo  aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Khalfan Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Ling’wenya ambao wote ni makomandoo wastaafu wa JWTZ kikosi namba 92KJ kilichopo Ngerengere.