Shahidi wa kwanza upande wa utetezi Adam Kasekwa (Mshitakiwa wa 2), amepata kigugumizi cha kujibu maswali aliyokuwa akiulizwa na Wakili wa Serikali Abdallah Chavula. Hayo yamejiri leo katika Kesi Na.16/2021 inayowakabili Freeman Mbowe na wenzake 3, ambapo shahidi huyo ametoa ushahidi wake mbele Jaji Mustapha Siyani katika Mahakama Kuu Division ya Uhujumu Uchumi na Rushwa Ni baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Adballah Chavula, alipomuuliza mshtakiwa huyo mahakama ichukue kauli ipi kati ya maelezo yake aliyowahi kutoa mahakamani hapo, akidai alitoa maelezo yake ya onyo katika Kituo cha Polisi Mbweni mkoani Dar es Salaam, kwa mateso na maelezo aliyotoa akidai, alichukuliwa maelezo yake baada ya kutishwa na sio kuteswa.
Swali hilo lilimpa Shahidi huyo tafakuri kubwa na kigugumizi kabla ya kulijibu, akidai wakati aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Arusha, ACP Ramadhan Kingai, alimsainisha karatasi yenye maelezo ya onyo hakumpiga bali alimtesa.Jibu hilo halikuiridhisha mahakama hiyo, ambapo Jaji Siyani alitoa nafasi nyingine kwa Wakili Chavula, kuuliza swali ili mshtakiwa huyo alielewe kisha alijibu kwa ufasaha. Wakili Chavula alimhoji tena shahidi huyo kwamba kauli ipi ni sahihi kati ya alikuwa anateswa na alitoa maelezo hayo baada ya kuteswa na ile aliyodai, alipofikishwa Dar es Salaam, hakuteswa bali alipewa karatasi yenye maelezo hayo na kuambiwa asaini na aweke maneno ya uthibitisho.Kasekwa alijibu kwa kusema kuwa , wakati anachukuliwa maelezo ya onyo hakupigwa bali alipata mateso ikiwemo ya kufungwa pingu.
Hata hivyo, Jaji Siyani alimtaka Kasekwa achague ajibu sahihi na kama atakuwa anakosea wakili wake, John Mallya atamsaidia.Pia, Jaji Siyani alisema majibu ya mshtakiwa huyo katika swali hilo ni muhimu, kwa kuwa mahakama hiyo inayategemea katika kutoa uamuzi.Wakili Mallya alinyanyuka na kumsaidia mteja wake, akidai mteja wake amejibu akidai hakupigwa na ACP Kingai, lakini hakumaanisha kama hakuteswa kwani hata kufungwa pingu ni mateso pia.Hata hivyo wakili Peter Kibatala, alinyanyuka na kusema ili kuondoa mkanganyiko huo, Wakili Chavula anatakiwa atafute namna bora ya kumuuliza swali shahidi huyo, badala ya kushindana.Kufuatia kauli hiyo ya Wakili Kibatala, Jaji Siyani alimhoji mshtakiwa huyo mahakama hiyo iandike kama hakupigwa mkoani Dar es Salaam, ambaye alijibu akidai ndiyo Dar es Salaam hakupigwa.Kasekwa alijibu akidai, alitoa maelezo bila ya mateso lakini alitoa maelezo chini ya mateso.
Majibu ya Kasekwa yaliwafanya waliokuwa ndani ya chumba hicho cha Mahakama kufurahia majibu ya Kasekwa na wengine wakimtazama Shahidi huyo ni kama mwenye uelewa mkubwa wa kujibu maswali ya Mawakili.Ikumbukwe kuwa Shahidi huyo ni mshtakiwa namba 2 kwenye kesi hiyo na upande wa Utetezi unategemea kuwa na mashahidi wengine watatu mbali na Kasekwa.Kasekwa alianza kutoa ushahidi wake Ijumaa iliyopita, tarehe 24 Septemba 2021, katika kesi hiyo ndogo iliyotokana na pingamizi la utetezi dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo, wakitaka yasitumike kama ushahidi wa jamhuri, ukidai yalichukuliwa kinyume cha sheria.Washatakiwa wengine ni Freeman Mbowe, Halfan Bwire Hassan na Mohammed Abdillah Ling’wenya.Shahidi anaendelea kutoa ushahidi.