Shahidi wa nne wa upande wa utetezi, Brenda Rupia, ameanza kutoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, akieleza namna mkutano wa chama wa Aprili 3, 2025 ulivyoandaliwa na kupinga madai kwamba mshtakiwa ndiye aliyeandaa mkutano huo.

Rupia, mwenye umri wa miaka 34, anayeishi Basihaya, Kata ya Bunju jijini Dar es Salaam, ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, nafasi aliyoteuliwa Machi 12, 2025 na Kamati Kuu ya chama hicho.
Lissu ambaye ni Mwanasiasa mashughuli wa Upinzani na mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Tanzania, anakabiliwa na kesi ya uhaini akidaiwa kutenda kosa la kuitishia Serikali, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code – PC) Rekebu ya mwaka 2023.
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa kutamka na kuandika (kuchapisha) mtandaoni maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Maneno hayo yanayodaiwa kuwa ya uhaini, Lissu alitamka kuwa : “Wanasema kitu kimoja hapa, msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Akiongozwa na Lissu katika kutoa ushahidi wake, Rupia alisema kabla ya kuteuliwa katika nafasi hiyo alikuwa Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) Wilaya ya Kinondoni, nafasi aliyokuwa ameishikilia tangu mwaka 2024.
Alisema kabla ya hapo aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Mwananyamala na baadaye kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bawacha wa Jimbo la Kinondoni.
Kitaaluma, Rupia alisema amesomea Shahada ya Sayansi ya Uhasibu (Bachelor of Science in Accounting) katika Chuo Kikuu cha Gloucestershire nchini Uingereza, ambako alisoma kuanzia mwaka 2009 hadi 2013.
Kabla ya kujihusisha zaidi na shughuli za kisiasa, alisema aliwahi kufanya kazi kama mhasibu katika kampuni ya TAZ KAZ iliyokuwa ikijishughulisha na uuzaji wa magari kwa kipindi cha mwaka mmoja, kabla ya kuacha ajira na kuanza biashara ya bidhaa za urembo, hususan nywele bandia (human hair).
Akieleza alichokijua kuhusu mkutano wa Chadema uliofanyika Aprili 3, 2025, Rupia alisema chama hicho kiliwaalika watia nia waliokuwa na mpango wa kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, mkutano huo ulihusu msimamo wa Chadema wa “No Reforms, No Elections”, uliodai kufanyika kwa marekebisho ya sheria za uchaguzi kabla ya uchaguzi.
Rupia alisema uamuzi wa kuitisha mkutano huo ulifanywa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, pamoja na Sekretarieti ya chama.
Alifafanua kuwa Sekretarieti ni chombo cha utekelezaji kinachoshughulikia shughuli za chama kila siku, kikijumuisha Katibu Mkuu, manaibu wake wawili pamoja na wakurugenzi wa chama.
Alisema baada ya uamuzi huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano aliwaandikia barua watia nia Machi 27, 2025, kuwaalika kwenye mkutano wa Aprili 3 katika Makao Makuu ya Chadema, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.
Rupia alisema baada ya hapo taarifa ya mkutano huo iliwekwa pia kwenye kurasa za chama na vyombo vya habari vikaalikwa kuripoti mkutano huo.
Katika hatua muhimu ya ushahidi wake, Rupia alipoulizwa kuhusu madai yanayomkabili Lissu kwamba ndiye aliyeandaa mkutano huo, alikanusha.
Alisema Lissu hakuwa mtu aliyeandaa mkutano wala aliyewaalika waandishi wa habari, bali alikuwa mzungumzaji aliyealikwa kuzungumzia msimamo wa chama wa “No Reforms, No Elections”.
Shahidi huyo pia alisema waandishi wa habari waliokuwepo kwenye mkutano huo walitoka katika vyombo mbalimbali, ikiwemo Chanzo TV, Mwanzo TV, Jambo TV, ITV na Mwananchi.
Alisema baadhi yao walifika wakiwa na kamera na vipaza sauti, huku wengine wakiwa na kalamu na karatasi kwa ajili ya kufuatilia na kuripoti mkutano huo.
Kuhusu kama waandishi hao walirusha mkutano huo moja kwa moja, Rupia alisema hawezi kuthibitisha hilo kwa sababu baadhi yao wanaweza kuwa walirekodi mkutano na kurusha baadaye au wasirushe kabisa.
Katika ushahidi mwingine, Rupia alisema Lissu alikuwa mzungumzaji mkuu wa mkutano huo na hakumwona akifanya shughuli nyingine zaidi ya kutoa hotuba kuhusu msimamo wa “No Reforms, No Elections”.
Akizungumzia madai kwamba Lissu alihusika kuchapisha mkutano huo kupitia Jambo TV, Rupia alisema madai hayo si ya kweli.
Alisema Lissu hakuwa mfanyakazi wa Jambo TV na kwamba hakuwa akifahamu kuwa kituo hicho kingefika kwenye mkutano huo.
Rupia pia alisema Lissu hakujua kwamba waandishi wa habari walikuwa wamealikwa kwenye mkutano huo.
Kuhusu umiliki wa maudhui yanayotengenezwa na chombo cha habari, shahidi huyo alisema kwa ufahamu wake, maudhui hayo huwa yanamilikiwa na chombo kilichoyatengeneza.
Kwa upande wa maudhui yaliyotengenezwa na Jambo TV kuhusu mkutano wa Aprili 3, 2025, Rupia alisema yalikuwa mali ya Jambo TV au Mkurugenzi wa chombo hicho.
Kwa leo shahidi huyo alihitimisha ushahidi wake kwa namna hiyo kutokana na muda wa Mahakama kuisha, hivyo kulazimika kesi kuahirishwa.
Hata hivyo itakumbukwa kuwa leo Septemba 7, 2026 ilipaswa kuwa mwisho wa kikao cha Mahakama kwa maana shauri lilipaswa kuisha leo, lakini imeshindikana kutokana na mwenendo wa ushahidi kutomalizika hivyo Mahakama imeongeza siku 14 kwa lengo la kuhakikisha shauri hilo linamalizika.
Katika kuhakikisha utekelezaji huo unafanyika ndani ya siku hizo zilizoongezwa Jaji Dastun Ndunguru aliwataka mawakili kuelekeza nguvu zao kwenye kesi hiyo na kuacha mambo mengine yasiyohusiana na mwenendo wa shauri.
Kesi imeahirishwa mpaka kesho Septemba 8,2026 saa tatu asubuhi ambapo shahidi wa nne ataendelea na ushahidi wake wa msingi