
Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, imeendelea leo Oktoba 9, 2025 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, masijala ndogo ya Dar es Salaam ambapo shahidi wa kwanza wa Jamhuri amemaliza kutoa ushahidi wake, hatua iliyomkaribisha shahidi wa pili, kuendelea na ushahidi wake.
Shahidi wa kwanza alihitimisha ushahidi wake leo baada ya kuhojiwa kwa maswali ya nyongeza na jopo la mawakili wa Serikali saba wakiongozwa na Wakili Renatus Katuga.
Katika mahojiano hayo, ambayo yameongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga alimtaka shahidi kufafanua kuhusu maelezo aliyotoa awali kuwa “kufanya uchochezi kwa nia ya kuitisha Serikali ni kosa la uhaini.”
Wakili Katuga: Uliulizwa kuhusiana na kwamba kufanya uchochezi ni uhaini, wewe ukasema ndiyo. Ulimaanisha nini?
Shahidi: Kufanya uchochezi kwa nia ya kuitosha Serikali ni kosa la uhaini, si uchochezi peke yake.
Wakili Katuga: Ulionyesha hati ya mashtaka iliyopo hapa Mahakama Kuu, uliulizwa kuhusu yale maneno yaliyo ndani ya nukuu. Ukaulizwa kama neno Serikali lipo, ukasema neno kama neno halipo, lakini baadaye ukasisitiza kwamba lipo. Ulimaanisha nini?
Shahidi: Neno Serikali kimaudhui kwenye hii hati ya mashtaka limo. Ukiangalia maneno haya… (Shahidi akayataja), ukitazama, neno hilo limo kwenye hati ya mashtaka kimaudhui, lakini si kama neno lililonukuliwa moja kwa moja.
Wakili Katuga: Pia uliulizwa kuhusu maneno “kuzuia uchaguzi ni kosa la uhaini”, ukajibu kwamba kuzuia uchaguzi kihalali si kosa la uhaini.
Shahidi: Nilimaanisha kuzuia uchaguzi kwa kufuata utaratibu wa kisheria, mfano kwa kwenda Mahakamani, si kosa. Lakini kuzuia uchaguzi halali kwa vitisho dhidi ya Serikali ni kosa la uhaini.
Wakili Katuga: Ulipoulizwa maswali kuhusu maelezo ya P, uliiambia Mahakama kwamba kwa mujibu wa maelezo hayo, aliyechapisha ni Tundu Lissu. Ukaulizwa nani ana password za Jambo TV, ukasema hujui. Tuambie, ulikuwa unamaanisha nini?
Shahidi: Maana yangu ni kwamba Mwenyekiti wa Chadema, kwa kitendo chake cha kuzungumza na waandishi wa habari, ni dhahiri alikusudia maneno yale yachapishwe.
Wakili Katuga: Uliulizwa sasa ni nani aliyepeleka hayo maneno mtandaoni, ukasema si mtu wa Jambo TV.
Shahidi: Nilikuwa namaanisha kwamba mtu wa Jambo TV ni mwandishi wa habari, ambaye Mwenyekiti wa Chadema ndiye aliyekuwa anaongea naye kwa lengo la maneno hayo yachapishwe mtandaoni.
Wakili Katuga: Uliposema chama cha upinzani kupinga Serikali kwa njia halali si kosa, ulikuwa unamaanisha nini?
Shahidi: Kama nilivyosema, chama cha upinzani kukosoa Serikali si kosa, isipokuwa kama kinatumia vitisho dhidi ya Serikali.
Baada ya shahidi huyo kumaliza maelezo yake, upande wa Jamhuri ulimleta shahidi wa pili, Inspekta John Kahaya ambaye ni afisa wa polisi mwenye umri wa miaka 45.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Job Mrema, Inspekta Kahaya alieleza kuwa ameajiriwa na Jeshi la Polisi tangu mwaka 2005, akihitimu mafunzo yake katika Chuo cha Polisi Zanzibar mwaka 2006 na kupangiwa Makao Makuu ya Polisi, Kitengo cha Upelelezi.
Shahidi huyo alisema kwa sasa anatekeleza majukumu yake katika dawati la upelelezi wa makosa ya mtandaoni, ambapo majukumu yake ni kufanya doria katika mitandao ya kijamii kama Facebook, X (zamani Twitter) na YouTube.
Akizungumza kuhusu tukio la Aprili 4, 2025, shahidi alisema akiwa kazini alibaini video iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Jambo TV yenye kichwa cha habari “Tundu Lissu uso kwa uso na watia nia majimboni, No Reforms No Election njia panda.”
“Nilipoiangalia video hiyo, nilisikia maneno yaliyokuwa na viashiria vya jinai, ikiwemo madai kwamba polisi wanaingia na vibegi vya kura feki na kwamba mahakama haziwezi kutoa haki kwa sababu majaji ni watu wa Rais,” alisema.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, maudhui hayo yalionekana kupotosha umma na kuashiria nia ya kuichafua Serikali.
“Niliona ni maudhui yanayoweza kuhamasisha uasi na hivyo nikayachukulia kama ushahidi wa jinai,” alisema.
Mrema: Ulijitambulisha kwamba wewe ni Inspekta Kahaya, afisa wa polisi. Tuambie, umeajiriwa lini?
Shahidi: Nimeajiriwa na Jeshi la Polisi baada ya kuhitimu mafunzo yangu mwezi Agosti 2005, na niliamaliza mafunzo hayo mwezi Februari 2006.
Mrema: Ulihitimu mafunzo hayo wapi?
Shahidi: Mafunzo hayo niliyapata katika Chuo cha Polisi Zanzibar.
Mrema: Ulijifunza nini katika mafunzo hayo?
Shahidi: Nilijifunza mbinu mbalimbali za kivita, sheria mbalimbali kama vile Sheria ya Ushahidi, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kazi za polisi, investigation skills pamoja na huduma ya kwanza.
Mrema: Eleza Mahakama, baada ya mafunzo hayo, ulipata nini?
Shahidi: Baada ya kumaliza mafunzo hayo nilitunukiwa cheti. Baada ya kuhitimu, nilipangwa Makao Makuu ya Polisi katika Kitengo cha Upelelezi.
Mrema: Unaposema Makao Makuu unamaanisha nini?
Shahidi: Namaanisha ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) katika Makao Makuu ya Polisi.
Mrema: Ilikuwa mwaka gani?
Shahidi: Ilikuwa mwaka 2006, na ilipofika mwaka 2020 nilihamishiwa katika Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni, kwenye Dawati la Doria Mtandaoni.
Mrema: Umeeleza kwamba ulianza kazi mwaka 2006, tueleze ulikuwa unafanya nini kati ya mwaka huo hadi 2020.
Shahidi: Kipindi cha mwaka 2006 hadi 2020 nilikuwa nafanya kazi ya upelelezi wa makosa mbalimbali ya jinai, kukamata watuhumiwa wa makosa hayo, kuandaa ushahidi, kuwafikisha watuhumiwa Mahakamani pamoja na kutoa ushahidi.
Mrema: Hicho kitengo cha upelelezi wa makosa ya mtandaoni kiko chini ya nani?
Shahidi: Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni kipo chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Mrema: Hiyo ofisi ya DCI kwa mwaka 2006 ilikuwa wapi?
Shahidi: Ofisi hiyo ilikuwa katika Makao Makuu ya Polisi, Dar es Salaam, lakini baadaye ilihamishiwa Dodoma.
Mrema: Kwa sasa ipo wapi?
Shahidi: Baada ya Serikali kuhamishia makao makuu yake Dodoma, ofisi hiyo pia ilihamishiwa mkoani Dodoma.
Mrema: Kwa sasa unatekeleza majukumu yako wapi?
Shahidi: Kwa sasa natekeleza majukumu yangu katika ofisi za zamani za Makao Makuu ya Polisi hapa Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine Shahidi aliongeza kuwa mnamo Aprili nne akiwa katika utekelezaji wa majukumu yake aliona picha mjongeo ambayo anadai kuwa ilikua na viashiria vya Jinai.
Mrema: Mnamo tarehe 4, mwezi Aprili, wewe ulikuwa wapi?
Shahidi: Aprili 4, 2025, majira ya saa 12 asubuhi, nilikuwa zamu kazini.
Mrema: Ieleze Mahakama, kwa tarehe hiyo, jambo gani lilitokea?
Shahidi: Mnamo Aprili 4, 2025, niliingia zamu majira ya saa 12 asubuhi. Baada ya kufika ofisini, niliandaa vitendea kazi vyangu — yaani kompyuta na huduma ya intaneti (internet access). Baada ya kuandaa vitendea kazi hivyo, niliwasha kompyuta mali ya Jeshi la Polisi kwa kutumia username na password yangu. Baada ya kuwaka, nilihakikisha kompyuta ipo katika hali nzuri inayoniwezesha kuendelea na majukumu yangu.
Mrema: Ieleze Mahakama, baada ya kukagua, nini kilifanyika?
Shahidi: Baada ya kukagua, nilibaini kuwa kompyuta hiyo ilikuwa katika hali nzuri ya kufanya kazi. Baada ya kuona hivyo, niliendelea na majukumu yangu ya kawaida ya doria mtandaoni, nikaanza kuperuzi mitandao ya kijamii. Nilipoingia katika mtandao wa YouTube, nilibaini machapisho mbalimbali ya picha mjongeo (video). Moja ya video hizo ilikuwa imechapishwa katika ukurasa uliosajiliwa kwa jina la Jambo TV.
Katika picha mjongeo hiyo, kulikuwa na maandishi yaliyosomeka: “Tundu Lissu uso kwa uso na watia nia majimboni — No Reforms No Election, njia panda.”
Mrema: Baada ya kuona video hiyo, ulifanya nini?
Shahidi: Baada ya kuona picha mjongeo hiyo, niliichezesha ili kusikiliza na kutazama maudhui yaliyokuwa yamechapishwa ndani yake.
Mrema: Kwa nini ulitaka kuiangalia video hiyo?
Shahidi: Kilichonifanya niangalie video hiyo ni baada ya kuona idadi kubwa ya watazamaji, takribani watu 39,000, na waliokuwa wamechangia (comment) walikuwa takribani 300.
Mrema: Ieleze Mahakama, kuhusiana na majukumu yako, yapo katika ngazi gani?
Shahidi: Majukumu yangu ni kuperuzi na kubaini makosa mbalimbali ya jinai yanayofanywa na watumiaji wa mitandao ya kijamii.
Akiwa anaperuzi ndio alipoiona picha mjongeo ambayo yeye anadai ina jinai ndani yake
Mrema: Ieleze Mahakama baada ya kukagua.
Shahidi: Baada ya kukagua, niliweza kubaini kwamba kompyuta ile inaweza kuendelea na kufanya kazi zangu za kila siku. Baada ya kuona hivyo, niliendelea na shughuli zangu za kuperuzi mitandao ya kijamii na niliingia mtandao wa kijamii wa YouTube. Baada ya kuingia katika mtandao ule, nilibaini machapisho mbalimbali ya picha mjongeo (video), moja ya chapisho hilo likuwa katika ukurasa uliosajiliwa kwa jina la Jambo TV. Katika picha mjongeo hiyo, lilikuwa limeambatanishwa na maneno: “Tundu Lissu USO kwa USO na Watia Nia Majimboni, No Reforms No Election, Njia Panda.”
Mrema: Sasa baada ya kuona, ulifanya nini?
Shahidi: Baada ya kuona picha mjongeo hiyo, niliichezesha ili kusikiliza maudhui yaliyochapishwa.
Mrema: Kwa nini ulitaka kuiangalia?
Shahidi: Kilichonifanya niiangalie video ile ni baada ya kuona ina watazamaji wengi, takribani 39, na watu walioshiriki kukoment walikua takribani 300.
Mrema: Ieleze Mahakama kuhusiana na majukumu yako, yapo kwa level gani kati?
Shahidi: Majukumu yangu ni kuperuzi na kubaini makosa mbalimbali ya jinai yanayofanywa na watumiaji wa mitandao hiyo.
Mrema: Ulibaini nini baada ya kuangalia video ile?
Shahidi: Baada ya kutazama maudhui yale, niliweza kubaini baadhi ya matamshi yenye viashiria vya jinai.
Mrema: Unaweza kueleza hivyo viashiria?
Shahidi: Baadhi ya matamshi yaliyo na viashiria vya jinai ni pale aliposema: “Kwa kuwa hatuna access na hizo servers za Tume, ndo hao mapolisi mnaowaona na vibegi vya kura feki.” Maneno mengine yaliyotamkwa na Tundu Lissu yalikuwa: “Majaji nao ni watu wa Rais, wao ni wa CCM, wanataka wapandishwe vyeo kwenda kwenye Mahakama za Rufani, kuteuliwa kwenye Commission na kwenye Tume, ndo kuna hela. Kwa hiyo Mahakamani hakuendeki.” Maudhui mengine aliyoyatamka ndugu Tundu Antipus Lissu: “Na mimi nataka niteuliwe katika kacheo fulani katika nchi hii na ninyi mnataka mteuliwe katika kacheo fulani; hali ilivyo, haliwezekani. Tufanyeje? Mkutano wetu unasema No Reforms No Elections. Wamesema kitu kimoja sahihi hapa; msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli, kwa sababu wamesema tutazuia uchaguzi, tutakinukisha sanasana.”
Mrema: Shahidi, ebu ieleze Mahakama, baada ya kusikiliza video hiyo, ulibaini nini?
Shahidi: Baada ya kusikiliza video ile, nilibaini matamshi yale yana viashiria vya jinai. Maneno aliyoyasema kuhusu askari kuingia na vibegi vya kura feki, niliona maneno yale yanapotosha umma. Pamoja na matamshi hayo, Tundu Antipus Lissu aliposema Mahakamani hakuendeki kwa sababu majaji ni watu wa Rais, niliweza kuona taarifa ile ina viashiria vya jinai kwa sababu kwenye kanuni za maadili ya utumishi wa umma inakataza watumishi kuwa wafuasi au wanachama wa vyama vya siasa. Aidha, majaji alivyotamka kwamba Mahakamani hakuendeki, ni kutoa taarifa ya uongo kwa umma na pia ni lengo la kuitishia Serikali.
Mrema: Ieleze Mahakama, baada ya kutazama ile video, kuna kitu kingine ulikibaini?
Shahidi: Alisema tutaenda kuzuia uchaguzi. Maneno mengine alitamka kwamba tutazuia uchaguzi kwa sababu tunahamasisha uasi na tutaenda kuuvuruga sanasana. Kwa matamshi haya, niliweza kuona kuna viashiria vya jinai kwa kuwa uchaguzi huandaliwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria; hivyo kuzuia uchaguzi kwa kuhamasisha uasi bila kufuata utaratibu wa kisheria au oda ya Mahakama. Nia yake ni kuitishia Serikali, ambayo ndiyo msimamizi wa sheria na kulinda mali.
Mrema: Baada ya kutizama maudhui yale?
Shahidi: Baada ya kutizama maudhui yale, nilichukua notebook kwa ajili ya kunote ukurasa wa Jambo TV uliochapisha maudhui yake pamoja na link inayohusu maudhui hayo.
Mrema: Shahidi, umekuwa ukitamka Tundu Antipus Lissu, unamfahamu?
Shahidi: Ndiyo, namfahamu.
Mrema: Unamfahamu vipi?
Shahidi: Namfahamu kama Mwanasheria, Wakili Msomi, na ni Mwenyekiti wa Chadema.
Mrema: Baada ya kuchukua kumbukumbu za hiyo video kwenye notebook yako, nini kilifuatia?
Shahidi: Nilimjulisha mkuu wangu wa kitengo kuhusiana na picha mjongeo hiyo, naam, Mkuu wa kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandao, Dawati la Upelelezi.
Mrema: Hiyo picha mjongeo ulimaliza kuiangalia saa ngapi?
Shahidi: Nilimaliza kuiangalia majira ya saa nne asubuhi ya tarehe 4 Aprili, 2025.
Mrema: Taarifa ulitoa muda gani?
Shahidi: Baada tu ya kumaliza kuicheza na kunote kwenye notebook yangu, ndipo nilipomjulisha mkuu wa kitengo.
Mrema: Baada ya kutoa taarifa hiyo, nini kilifuatia?
Shahidi: Baada ya kutoa maudhui yake, nilielekezwa kwenda Polisi Kanda Maalum ya DSM kwa ajili ya kumjulisha Afande SSP George Bagemu juu ya maudhui yale.
Shahidi huyo alisema aliendelea kufuatilia mwenendo wa video hiyo, ambapo kufikia Aprili 7, 2025, idadi ya watazamaji ilikuwa imeongezeka hadi zaidi ya 52,000.
Kesi imeahirishwa mpaka kesho Oktoba 10, 2025 kwa ajili ya kuendelea kutolewa ushahidi ambapo Tundu Lissu anaejiwakilisha mwenyewe kwenye kesi hiyo atamuhoji maswali ya dodoso shahidi.