Takriban miezi miwili baada ya mapinduzi ya Januari 24, ghasia zimerejea nchini Burkina Faso. Shambulio la watu wanaoshukiwa kuwa wanajihadi limesababisha vifo vya wanajeshi 13 na wanane kujeruhiwa katika jeshi la nchi hiyo siku ya Jumapili karibu na eneo la Natiaboani, mashariki mwa nchi hiyo
Taarifa ya Jeshi la Burkina Faso imesema Kikosi cha kijeshi kilichokuwa katika operesheni ya usalama katika eneo la Mashariki kilikabiliana na kundi la watu wenye silaha takriban kilomita ishirini mashariki mwa eneo la Natiaboani, jana Jumapili, Machi 20, 2022
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa Wakati wa mapigano, askari kumi na watatu waliuawa kwa bahati mbaya na wengine wanane walijeruhiwa,hata hiyo ” jeshi linendelea kuhakikisha kuwa washambuliaji wanaangamizwa.
Natiaboani ni mji wa mashambani ulioko takriban kilomita sitini kusini mwa Fada N’Gourma, mji mkuu wa eneo la Mashariki, unaolengwa mara kwa mara na mashambulizi ya makundi yenye silaha tangu 2018.
Kulingana na shirika la habari la Burkina, takriban vijana kumi na watano walitekwa nyara na watu waliokuwa na silaha baada ya shambulio huko Nagré, karibu na mlji wa Natiaboani, siku ya Ijumaa
Katika siku kumi, hili ni shambulio la sita lililorekodiwa, kaskazini na mashariki mwa Burkina Faso. Jumla ya raia 23 na askari 25 waliuawa katika mashambulizi haya.
Mnamo Januari 24, Luteni-Kanali Paul-Henri Damiba alimpindua Rais Roch Marc Christian Kaboré, ambaye mara nyingi alishutumiwa kwa kutofanya kazi katika kukabiliana na ghasia za wanajihadi.
Lakini baada ya utulivu, rais mpya, ambaye ameweka vita dhidi ya wanajihadi kuwa kipaumbele, anajikuta akikabiliwa na mashambulizi mabaya.
Mbali na Mali na Niger, Burkina Faso imekumbwa tangu mwaka 2015 na ghasia zinazotokana na vmakundi ya wanajihadi, yenye mafungamano na Al-Qaeda na kundi la Islamic State, ambalo limeua zaidi ya watu 2,000 nchini humo na kuwalazimisha angalau watu milioni 1.7 kutoroka makazi yao.