Mwanzo Tv

Nairobi Kenya

+254 7

24/7 Customer Support

Mon - Fri: 9:00 - 17:30

Online Media always open

Shujaa wa Mau Mau – Field Marshall Muthoni akatwa nywele alizofuga kwa miaka 70

Field Marshall Muthoni akikatwa nywele na Mama Ngina Kenyatta

Mashujaa wa vuguvugu la Maumau lililopigania uhuru wa Kenya kutoka kwa mkoloni Uingereza wazidi kuenziwa hadi leo.

Wanawake kwa wanaume walishiriki katika kumfurusha mkoloni ila mwanamke anayefahamika zaidi na aliyepewa jina la heshima la Field Marshall ni Muthoni ambaye kwa miaka 11 alikuwa msituni akipigana na mkoloni.

Mwaka wa 1963 Kenya ilipopata uhuru alijitokeza kutoka msituni akiwa amebeba shoka, bunduki kati ya silaha nyingine.

Field Marshall Muthoni alijiunga na vuguvugu la maumau akiwa na umri wa miaka 20. Kazi yake ya kwanza aliyofanya ilikuwa kuwa jasusi, na alifanya kazi hiyo kwa takriban miaka miwili.

Field Marshall Muthoni, alipojiunga na maumau

Kazi hiyo ilimletea matatizo makubwa na mateso kutoka kwa mkoloni kiasi cha kupigwa kichapo cha umbwa, inasemekana majeraha alityopata yalimpatia matatizo ya uzazi na hakuwahi kupata watoto baada ya mimna zake mbili kuharibika.

Baada ya Kenya kupata uhuru wake,alijishughulisha na biashara ikiwa kuuza limau sokoni.

Field Marsahll Muthoni anajivunia juhudi alizotoa katika kupigania uhuru wa Kenya, na ili kuweka kumbukumbu ya muda huo, machozi na damu iliyomwagika mikononi mwa mbeberu, hakuwahi kukata nywele zake alizofuga kwa takriban miaka 70.

Alifuga nywele hizo zilizokuwa na urefu wa futi 6, na kuahidi atazinyoa tu, ile siku ambapo Kenya itakuwa huru kweli.

Ila siku ya Jumamosi katika sherehe iliyofanyika nyumbani kwake katika mtaa wa Pembe Tatu mjini Meru na kushuhudiwa na aliyekuwa mke wa Rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta, nywele hizo ambazo zimeashiria mapigano ya muda mrefu ya kupatikana kwa uhuru wa Kenya, zilianguka moja baada ya nyingine zilipokatwa na Mama Ngina Kenyatta.

Nywele hizo zilifungwa kwenye bendera ya Kenya na kutiwa chondoni na kupewa shujaa huyo.

Field Marshall Muthoni Kirima, ni kati ya mashujaa ambao walijitolea kwa hali na mali katika kuona kuwa Kenya inakuwa huru.