Siasa za visasi zadaiwa kukitafuna CHADEMA, G55 watangaza kujiondoa

Kundi la viongozi wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), maarufu kama G55, limetangaza rasmi kujiondoa katika chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, likidai kukithiri kwa ukiukwaji wa katiba, ubaguzi na siasa za visasi zinazoendeshwa na uongozi wa sasa.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam leo, aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA upande wa Bara, Benson Kigaila, amesema hatua hiyo inatokana na kukosekana kwa mwelekeo ndani ya chama hicho pamoja na kupuuzwa kwa ushauri wao wa ndani ya chama kwa muda mrefu.

“Tumeamua kujiondoa CHADEMA kwa sababu hatuwezi kushuhudia chama kikifa mbele ya macho yetu halafu tuje kulaumiwa kuwa tulikuwa sehemu ya mipango ya kukiangamiza,” alisema Kigaila.

Akiwa ameambatana na viongozi wengine wa zamani, wakiwemo Salum Mwalimu (aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar) na Catherine Ruge (aliyekuwa Katibu wa Baraza la Wanawake CHADEMA), Kigaila aliongeza kuwa kundi hilo litatafuta jukwaa jingine muafaka la kuendeleza harakati za kisiasa nje ya CHADEMA, huku wakibainisha wazi kutokuwa na mpango wa kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwa upande wake, Salum Mwalimu alisema kuwa licha ya wao kuwa miongoni mwa waliounda mkakati wa kisiasa wa “No Reform, No Election,” wamevunjika moyo kuona kampeni hiyo sasa inatumika kama kisingizio cha kukwepa majukumu ya chama.

“Chama hakina fedha, hakina vikao, lakini kila wakati ukiuliza unaambiwa ‘No Reform, No Election’. Je, hiki ndicho chama kitasimamia tu bila ajenda nyingine za msingi?” alihoji Mwalimu.

Mwalimu alibainisha kuwa kati ya wajumbe 12 wa zamani wa Sekretarieti ya CHADEMA, wanane tayari wamekubaliana kuachana na chama hicho.

Katika mkutano huo pia, Catherine Ruge alitangaza kujivua uanachama wa CHADEMA, akisema hana tena imani na chama hicho kutokana na kile alichokiita “mgogoro wa kimawazo” unaoendelea ndani ya chama.

“Hakuna tena mwelekeo ndani ya CHADEMA. Watu wamegawanyika, hakuna mawasiliano ya dhati, na kila mwenye mtazamo tofauti anachukuliwa kama msaliti,” alisema Ruge.

Viongozi hao waliwalaumu baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho kwa kuendeleza siasa za visasi na ubaguzi, hasa kwa wale waliomuunga mkono aliyekuwa Mwenyekiti Freeman Mbowe wakati wa uchaguzi wa ndani uliofanyika Januari mwaka huu.

G55 ni kundi la viongozi waliowahi kushika nafasi nyeti ndani ya CHADEMA, lakini ambao katika miaka ya karibuni wamekuwa wakionyesha tofauti za wazi za kimtazamo na uongozi uliopo madarakani sasa.

Hatua yao ya kujiondoa inazidi kuibua maswali kuhusu mustakabali wa CHADEMA na mshikamano wa ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu ujao.