Siku 68 za Lissu gerezani, aeleza masaibu anayopitia

“Haki zangu za msingi zimekiukwa, sasa nitajitetea mwenyewe.”

Haya yalikuwa maneno mazito ya kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, aliyoyatoa mahakamani Jumatatu Juni 16, akieleza hali ya sintofahamu na mateso anayodai kupitia akiwa mahabusu kwa zaidi ya miezi miwili.

Kauli hiyo, iliyojaa msisitizo, imezua hofu mpya miongoni mwa watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati wa sheria, na jumuiya ya kimataifa kuhusu mwenendo wa haki jinai nchini humo.

Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa hadhara huko Mbinga, mkoani Ruvuma, ambapo alikuwa akiendesha kampeni ya kisiasa iitwayo “No Reforms, No Election”.

Anakabiliwa na mashitaka ya uhaini na uchochezi, ambayo kisheria katika shtaka la Uhaini iwapo atakutwa na hatia anaweza kuhukumiwa adhabu ya kifo.

-Amefungwa Kwenye Death Row Bila Kuhukumiwa-

Licha ya kutohukumiwa, Lissu amedai amekuwa akishikiliwa kwenye eneo maalum la wafungwa wanaosubiri kunyongwa (death row) ndani ya Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam.

“Ninakaa katika sehemu ya ‘special room’ — pale wanapokaa waliohukumiwa kunyongwa. Ninalindwa masaa 24, siwezi kushiriki ibada, siwezi kuzungumza kwa faragha na mawakili wangu. Sina hata hukumu bado, lakini natendewa kama nimeshapewa hukumu ya kifo,” alisema Lissu mbele ya Hakimu anayesimamia kesi ya Uhaini, Franco Kiswanga

Katika hali ya kushtua zaidi, Lissu amedai kwamba kwa siku zote 68 za mahabusu, hajawahi kuruhusiwa kuonana au kuzungumza faragha na mawakili wake zaidi ya 30 waliokuwa tayari kumtetea.

“Wamekuwa wakija gerezani, lakini hawaruhusiwi kuniona faragha. Tunawasiliana kwa simu ya gereza, hakuna kubadilishana nyaraka, hakuna maandalizi ya kweli ya utetezi,” alisema.

Kulingana na Kanuni ya 13 ya Sheria za Usimamizi wa Magereza za mwaka 1987, kila mfungwa au mahabusu ana haki ya kuonana na wakili wake kwa faragha. Hii pia inalindwa na Sheria ya Kimataifa kupitia Kanuni za Mandela (Mandela Rules) kuhusu haki za wafungwa.

-Adai kukosa haki ya kuabudu-

Lissu, ambaye ni Mkristo, alieleza pia kuwa ameendelea kunyimwa haki ya kuhudhuria ibada, hata katika sikukuu za kidini kama Ijumaa Kuu na Pasaka.

“Wafungwa wengine wote wanaruhusiwa kusali. Mimi pekee nimezuiwa. Kila Jumapili ninaomba, wanakataa. Hii ni haki ya msingi kwa kila binadamu, hata akiwa gerezani,” alisema Lissu, huku akisisitiza kuwa amekuwa akiomba ruhusa tangu alipoingia Ukonga, lakini bila mafanikio.

Wataalam wa Sheria wameeleza kuwa madai hayo ni ya “kusikitisha na hatari kisheria” na kwamba Serikali iko katika ukiukwaji wa moja kwa moja wa Katiba na Sheria za Kimataifa

“Kama kweli amenyimwa mawasiliano ya faragha na mawakili wake na haki ya ibada, basi Serikali iko katika ukiukwaji wa moja kwa moja wa Katiba na sheria za kimataifa. Hizi ni haki za msingi zisizoweza kuporwa kwa mtu yeyote,” 

Wanaharakati wa Haki za Binadamu wameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu mwenendo wa kesi ya Lissu, huku wakidai haki kutendeka na si kuendeleza ukandamizaji

“Huu ni muendelezo wa kuwakandamiza wapinzani kisiasa. Kumnyima mahabusu haki ya mawasiliano ya kisheria na ibada ni uvunjifu wa haki wa kiwango cha juu,” 

-Aamua Kujitetea Mwenyewe Mahakamani-

Lissu alitangaza rasmi kuwa atajitetea mwenyewe mahakamani, baada ya kukosa fursa ya kuandaa utetezi wake kwa ushirikiano na mawakili wake.

“Nimeamua kuwatua mzigo huu mawakili wangu. Mimi ni wakili wa Mahakama Kuu kwa miaka 22. Sioni sababu ya kuendelea kulazimisha kuwa na mawakili wakati haki hiyo imevunjwa. Nitajitetea mwenyewe,” alisema Lissu kwa msisitizo.

Kesi ya Lissu imekuja katika kipindi nyeti ambapo Tanzania inakaribia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Chama chake cha Chadema tayari kimeshatangazwa kutoidhinishwa kushiriki uchaguzi, baada ya kugoma kusaini mwongozo wa maadili ya uchaguzi waliouita wa “upendeleo”.

Wachambuzi wengi wa siasa wanasema kuwa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan unaanza kurudia mbinu za kiimla zilizokuwa zikitumika wakati wa Rais hayati John Magufuli.

Katika mwezi Mei, wanaharakati wawili kutoka Kenya na Uganda waliripotiwa kutiwa mbaroni walipokwenda Tanzania kuhudhuria kesi ya Lissu Mahakamani na baadaye kudai waliteswa na kudhalilishwa kijinsia wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola.

Kwa sasa, kesi ya Lissu ile ya Uhaini bado haijafikia hatua ya kuanza kusikilizwa rasmi (Committal), na Mahakama hapo jana iliahirisha kesi hiyo hadi Julai Mosi, 2025 majira ya saa tatu asubuhi.

Hata hivyo, mashinikizo ya kitaifa na kimataifa yanaendelea kuongezeka, yakitaka Lissu aachiwe 

“Tunafuatilia kwa karibu. Hii siyo kesi ya mtu mmoja, ni kipimo cha dhamira ya taifa letu kwa haki, uhuru na utawala wa sheria,”