Mwanzo Tv

Nairobi Kenya

+254 7

24/7 Customer Support

Mon - Fri: 9:00 - 17:30

Online Media always open

Simbachawene: Serikali haitarudisha makao yake makuu jijini Dar es salaam.

Serikali imetangaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan hana mpango wa kurudisha makao makuu ya nchi jijini Dar es Salaam badala yake anaendelea kuimarisha jiji la Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Uratibu George Simbachawene ambaye amesema kuwa, ziko taarifa za kwamba Rais anarudisha tena makao makuu yalikokuwa.

Ametoa kauli hiyo wakati akitoa ufafanuzi kuhusiana na maswali ya nyongeza ya wabunge baada ya Mbunge wa Ukonga Jelly Silaa kuuliza swali la msingi akitaka kujua iwapo Serikali haioni umuhimu wa kutenga siku za kutoa huduma kwenye Ofisi za Dar es Salaam ili kupunguza gharama kwa wateja wanaosafiri kufuata huduma Dodoma.

“Nataka niwaambie Watanzania kwamba, Rais ana nia njema sana na Dodoma, hana mpango wa kurejesha makao makuu Dar es Salaam, ndiyo maana ametenga fedha nyingi kujenga majengo ya Wizara lakini fedha zinazokuja Dodoma ni nyingi kuliko mikoa mingine ni kwa sababu hiyo,” amesema Simbachawene.

Katika hatua nyingine Waziri huyo amesema kuwa anakusanya taarifa za taasisi muhimu ambazo hazijahamisha makao yake kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na kwamba baada ya hapo atatoa kauli ya Serikali.

Akijibu swali la Silaa, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Ummy Nderiananga amesema pamoja na Serikali kuhamishia ofisi za Makao Makuu yake Dodoma, bado huduma zote zimeendelea kupatikana Dar es Salaam kama ilivyo kwa mikoa mingine nchini.

Nderiananga amesema huduma kwa umma zitaendelea kuimarishwa na kutolewa katika maeneo yote nchini ikiwemo Dar es Salaam.

“Pamoja na hayo, Serikali inaendelea na maboresho ya mifumo ya utoaji huduma kwa Umma kwa njia ya kieletroniki ili kupunguza ulazima wa wateja kusafiri au kufuata huduma hizo ofisini,” amesema Nderiananga.

Naibu Waziri amesema mpango wa kuhamia Dodoma hauathiri wingi wa watu waliopo Dar es Salaama na kutolea mfano wa nchi za Nigeria na Afrika Kusini ambao makao makuu yao yapo katika miji midogo ambayo haina watu wengi.