Soko la Njombe kuwa na kituo maalum cha kulelea watoto

Rais Samia Suluhu Hassan ameulekeza uongozi wa Mkoa wa Njombe kuweka kituo maalumu cha kulelea watoto katika soko kuu la Njombe kwa ajili ya watoto wa wanawake wanaofanya biashara kwenye soko hilo.

 Rais Samia ametoa agizo hilo leo Jumatano Agosti 10, 2022 alipotembelea na kuzindua soko hilo la kisasa akiwa ziarani mkoani Njombe.

“Nimepita hapa nimeona wanawake wengi wana watoto wadogo, wapo wanaowabeba mgongoni, wengine wanacheza chini mama zao wanaendelea na biashara.

“Ninachoona kuna haja ya kuwa na eneo maalum ambalo litawekwa kituo cha kulelea watoto ili kuwapa nafasi wazazi wao kuendelea na biashara,” amesema.

Hata hivyo, Rais Samia amewataka wanawake watakaokitumia kituo hicho kuwa tayari kuchangia huduma za kuwatunza watoto hao.

“Tukubaliane lazima tuchangie kidogo, maana watakuwepo watoa huduma na hata hayo mahitaji ya watoto ni vyema tukawa tayari kuchangia,” amesema Rais Samia.

Akizungumzaia ujenzi wa soko hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa amesema ujenzi wa soko hilo umegharimu shilingi bilioni 10.2.

Waziri Bashungwa amesema “Soko hili litawasaidia wafanyabiashara kufanya bishara zao mahali pazuri, hasa wajasiriamali.

“Mjasiriamali mdogo atalipa Sh10, 000 kwa kila mwezi kwa upande wa vizimba na hiyo ndio dhamira na maelekezo ya Rais Samia anapozungumzia kuweka maziringa rafiki kwa wafanyabiashara ndogondogo” amesema Bashungwa.

Soko hilo la kisasa lina ukubwa wa mita za mraba 9,186 lina sakafu (floors) tatu na Soko lina mifumo na sehemu mbalimbali yakiwemo maduka 162, meza za biashara 407, vyoo 47, migahawa 2, stoo 6, vizimba vya kuku 27, machinjio ya wanyama wadogo, sehemu za huduma za kibenki 2, ofisi za utawala 2, mfumo wa maji safi na maji taka, kisima kirefu cha maji.