Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amewataka viongozi wa Serikali ya nchi hiyo kuzima magari yao pindi wanaposhuka badala ya kuyaacha kwa muda mrefu yakiwa yanaendelea kunguruma huku wao wakiwa wanaendelea na shughuli zingine.
Dk Tulia amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma huku akiwashauri viongozi wa Serikali nchi nzima isipokuwa wanaoruhusiwa kiitifaki, kufanya hivyo akisema kuwa utekelezaji wa agizo hilo utasaidia kubana matumizi ya mafuta ya Serikali.
Amesema kuwa magari ya mawaziri na naibu mawaziri yanaachwa yakiwa yanawaka nje ya ukumbi wa bunge wakati wao wakiwa ndani ya Bunge hivyo kutaka yawe yanazimwa.
Amesema kuna juhudi zinazofanywa za kubana matumizi ya Serikali lakini magari ya viongozi wakiwemo manaibu mawaziri na mawaziri yanaendelea kuwaka nje ya ukumbi wakati mawaziri wapo ndani wanaendelea na vikao vya Bunge.
Amesema anatamani magari ya viongozi yanaposhusha viongozi nchini sio tu bungeni bali nchi nzima ukiacha wale kwa itifaki yao magari yanapaswa kuendelea kuwaka yanazimwa na dereva anashuka kwenye gari.
“Kwasababu matumizi ya fedha kwenye mafuta yanakuwa makubwa sana kwasababu ya magari kuendelea kuwaka wakati kiongozi hayupo kwenye gari ameshashuka ana mkutano was aa mbili, gari inaendelea kuwaka,” amesema Dk Tulia
Dk Tulia ametaka Serikali kulitazama jambo hilo na wangetamani waone mabadiliko katika eneo hilo ili matumizi ya mafuta katika Serikali yapungue.
“Hili ni la muhimu kwasababu hata sisi tunapoendesha magari yetu binafsi ukikwama kidogo tu katika foleni unazima sasa iweje kiongozi wa Serikali umemshusha kwa ajili ya kwenda katika mkutano unamsubiria kwenye gari ukiwa umewasha gari?”amehoji.
Amesema kwa kufanya hivyo ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali.