Sugu aishutumu CCM kwa madai ya uporaji wa uchaguzi, ataka uwajibikaji wa matumizi ya nguvu

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, ametoa tuhuma nzito dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akidai kuwa hakikushinda uchaguzi kwa ridhaa ya wananchi bali kilipora ushindi huo kwa kutumia nguvu ya dola.

Akizungumza kuhusu hali ya siasa na demokrasia nchini, Sugu alisema matumizi ya nguvu, hususan silaha, ni kinyume na misingi ya uchaguzi huru na wa haki. Alisisitiza kuwa mshindi halali wa uchaguzi anapaswa kuapishwa hadharani mbele ya wananchi ili kuthibitisha uhalali wa ushindi wake.

Kwa mujibu wa Sugu, matumizi ya vyombo vya dola katika michakato ya uchaguzi yanaashiria kukosekana kwa nia ya dhati ya kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa haki, hali ambayo, alisema, imeifanya CHADEMA kutathmini upya ushiriki wake katika baadhi ya michakato ya kisiasa.

Akirejea matukio ya Oktoba 29, 2025, mwanasiasa huyo alisema yaliyotokea siku hiyo hayajawahi kushuhudiwa, hata katika nchi zenye mifumo ya kiimla. Alidai kuwa matumizi makubwa ya nguvu na silaha ni doa katika historia ya siasa na utawala nchini.

“Yaliyotokea Oktoba 29, jambo la kwanza lazima kuwe na uwajibikaji. Haiwezekani mambo yote yale yametokea na hakuna hata mtu mmoja aliyewajibika. Tunahitaji watu wakiri ni nani aliyeamuru bunduki zipigwe,” alisema.

Aliongeza kuwa silaha zilizotumika si za raia, na iwapo zilitumika bila udhibiti, basi kuna haja ya kuwajibika kwa waliopaswa kusimamia usalama wa nchi. “Hata kama ni za mtaani, bado kuna mtu anapaswa kuwajibika kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo,” alisisitiza.

Sugu alieleza kuwa chama chake kitaendelea kusimama kudai haki za wananchi na kusukuma mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi ili kuhakikisha viongozi wanapatikana kupitia sanduku la kura, na si kwa nguvu ya silaha.

Aidha, aligusia masuala ya kisiasa yanayokihusu chama chake, akisisitiza kuwa kinachohitajika ni kurejea kwenye misingi ya haki na ukweli, huku akidai kuwa baadhi ya kesi zinazokikabili chama hicho zina lengo la kukizuia kufanya shughuli zake za kisiasa.