Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) imesema asilimia 60 ya kundi balehe la vijana wa kati ya miaka 15-24 walipima VVU na kujua hali zao kwa mwaka 2020.
Akizungumza na wanahabari hii leo Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini Tacaids, Laiser Nyangusi, amesema pamoja na kwamba asilimi 60 waliweza kupima kujua afya zao lakini bado kuna kundi la asilimia 40, ambalo hadi sasa halijajua hali zao kiafya.
“Takwimu hizo zinaonyesha bado kundi la asilimia 40 halijajua hali zao, lakini imeonyesha maambukizi hayo yanaenea kwa kasi zaidi kwa kundi la wasichana balehe umri wa miaka 15-24 kwa asilimia 2.1 ikiwa ni mara tatu zaidi ya vijana wa kiume kwa asilimia 0.6,” amesema Nyangusi.
Hata hivyo, katika matokeo hayo kundi la wasichana balehe na wanawake vijana lilikuwa mara mbili au tatu ya vijana wenzao wa kiume kwenye maambukizi.
Nyangusi amesema kati ya wenye VVU wapya 77,000 waliokutwa na maambukizi mapya mwaka 2019, asilimia 28 walikuwa na miaka 15 mpaka 24 na kati ya hao asilimia 67 walikuwa wasichana balehe na wanawake vijana huku wavulana wakiwa asilimia 23.
Aidha amesema wasichana wengi wanaathirika kutokana na ndoa za kulazimishwa ambazo zinawaweka hatarini kupata mimba zisizotarajiwa, utoaji mimba na maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo VVU.