Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Mbeya inawashikilia watu 40 kwa tuhuma za kuhusika kwenye wizi wa shilingi milioni 450 ambazo ni fedha za umma.
Kukamatwa kwa watu hao kumekuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaja ubadhilifu wa fedha mkoani Mbeya
Akizungumza leo Jumatatu Agosti 28, 2023 Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Denis Mwila amesema tuhuma zilizotajwa na Rais Samia ni za kweli ambapo watu 40 wakiwamo Madiwani, Wataalamu wa Tehama (IT), Watumishi na Watendaji wa kata wanashikiliwa na tayari baadhi yao wamefikishwa mahakamani.
Amesema hata kabla ya Rais kulizungumza, tayari walishaanza kulifanyia kazi tangu Julai 12, 2023 na kwamba mfumo huo wa ‘uchotaji’ fedha ulianza tangu 2018 na jumla ya Sh450 milioni zimeibiwa katika miaka mitano katika maeneo ya Mbeya, Njombe, Rukwa, Songwe na Ruvuma.
“Chanzo cha wizi huu ni mfumo unaotoka Dar es Salaam, ambapo kamati ya usalama Mkoa wa Mbeya tulifika huko na kumkamata mhusika na mfumo wake, lakini wamo Madiwani, Watumishi, Watendaji, Wataalamu wa Tehama na wakusanya ushuru na tayari baadhi wameshafikishwa mahakamani na wengine uchunguzi unaendelea chini ya Takukuru na wataendelea kufikishwa na wengine huko,” amesema.
“Maagizo ya Rais tunayafanyia kazi hakuna atakayebaki salama, na waliokamatwa ni wale wa Wilaya ya Mbarali, Mbeya Jiji, Mbeya Vijijini, Rungwe, Tunduma, Ileje, lakini tunaendelea na uchunguzi kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria,” amesema Mwila.
Hata hivyo imeelezwa kuwa Takukuru ambao wanahusika na watuhumiwa hao, watafafanua kujua wangapi na kina nani hadi sasa wamefikishwa mahakamani na ambao wanaendelea na uchunguzi juu ya tuhuma hizo kwa hatua zaidi.