Wizara ya TAMISEMI, imeidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 535.6, sawa na asilimia 41.1 ya fedha zote kati ya shilingi Trillion 1.9, fedha ambazo zimetolewa na Shirika la Fedha Duniani IMF, kwa ajili ya kukabliana na athari za UVIKO-19.
Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu, amesema kiasi hicho cha fedha walichokipata katika wizara hiyo, kimeelekezwa kwenye maeneo ya vipaumbele vinavyogusa wananchi moja kwa moja kwa ajili ya kuwaondolea kero katika kuzifikia na kuzipata huduma za afya, elimu na uwezeshaji wananchi kiuchumi, vilevile kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19’.
“Kwenye elimu fedha hizi tunazielekeza kujenga mabweni 50 kwa wanafunzi 4,000 wenye uhitaji maalam, mabweni haya yatatumia Sh4 bilioni na kila bweni litagharimu Sh80 milioni na ujenzi huo utafanyika katika mikoa yote 26,” – amesema Waziri Ummy
Ummy ameongeza kuwa kwa sasa kuna uhaba wa vyumba vya madarasa 12,000, hivyo kupitia mpango huo wa Maendeleo kwa Ustawi,Serikali itajenga vyumba vyote vya madarasa vinavyohitajika kwa ajili ya Kidato cha kwanza 2022. Ukamilishaji wa madarasa hayo utawezesha wanafunzi 600,000 kupata vyumba vya kusomea.
Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu
Wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2022 ni 1,022,936 huku mahitaji ya vyumba vya madarasa ni 20,535 ambavyo havilingani na idadi ya vyumba vya madarasa 8,535 vitakavyoachwa wazi na wanafunzi 422,403 wa kidato cha nne watakaofanya mtihani Novemba 2021.
Pamoja na hayo Ummy amesema fedha hizo pia zitakwenda kwenye huduma za afya ya msingi ambazo zitatumika shilingi bilioni 226.68, ambapo serikali inatarajia kuanzisha huduma za dharura katika hamashauri 75 na kujenga majengo ya huduma za wagonjwa mahututi 25 katika halmashauri 25 za kimkakati.
“Tunakwenda kununua mitambo 60 ya huduma ya mionzi, si halmashauri zote zitapata, tumeangalia hospitali za halmashauri ambazo hazina na kila mashine tunatarajia itagharimu Sh420 milioni kwahiyo tutatumia Sh25.2 bilioni kwa ajili ya kuweka mashine hizo,” – amesema Waziri Ummy Mwalimu
Fedha hizo zinajumuisha mkopo nafuu usio na riba kupitia dirisha la Rapid Credit Facility (RCF) wa jumla ya dola za Marekani milioni 189.08; na mkopo nafuu wenye riba ndogo kupitia dirisha la Rapid Financing Instrument (RFI) wa dola za Marekani milioni 378.17.