Tanzania kuchunguza tuhuma za wanafunzi kufundishwa vitendo vya ulawiti

Serikali ya Tanzania imetuma timu maalum kwenda mkoani Kilimanjaro nchini humo kuchunguza tuhuma za wanafunzi kufundishwa vitendo vya ulawiti vinavyodaiwa kufanyika katika baadhi ya shule mkoani humo.

Hivi karibuni vyombo vya habari nchini Tanzania viliripoti taarifa juu ya shule kutoa mafundisho ya ulawiti kwa wanafunzi katika shule hizo

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda, amesema jambo hilo wamelichukuliwa kwa umuhimu mkubwa na tayari timu inayoongozwa na kamishna wa elimu, mwanasheria wa wizara na Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora imeanza kufatilia suala hilo ili kubaini ukweli ili hatua zichukuliwe.

 “Tumeshtushwa sana na jambo hilo, tumelichukua suala hili kwa umuhimu mkubwa tumeongea na Mkuu wa Mkoa na kama kuna jinai yeyote basi hatua za kisheria zichukuliwe mara moja,” amesema Waziri Mkenda.

Ameongeza kuwa wizara ya Elimu itatoa namba maalumu, ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa za vitendo hivyo vinavyochafua taswira ya elimu, kuondoa imani ya wazazi kwa shule na inaharibu vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa.

 “Katibu Mkuu atatangaza namba ambayo mtu yeyote akijua kuna vitendo kama hivyo kwenye shule au chuo chochote nasi tutaifanyia kazi kwa kufanya uchunguzi ili kudhibiti vitendo hivyo,” ameeleza Prof.Mkenda. 

Katika kuweka mipango endelevu ya kudhibiti vitendo hivyo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inashirikaina na wizara nyingine za kisekta katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii, ikiwemo maeneo ya shule na vyuo nchini.